Serikali yapendekeza mabadiliko makali Sheria ya Takwimu

Nuzulack Dausen 0453Hrs   Agosti 21, 2018 Habari
  • Maboresho hayo yanataka mtu aliyethibitishwa na NBS kufanya utafiti kupata idhini ya ofisi hiyo kabla ya kuwasilisha matokeo hayo kwa umma.
  • Iwapo maboresho hayo yatapitishwa na Bunge kama yalivyo, itakuwa ni kosa kukosoa takwimu kuwa siyo sahihi.
  • Maboresho hayo pia yamelenga kufuta cheo cha Mkurugenzi Mkuu wa NBS na kuanzisha cheo cha Mtakwimu Mkuu.
  • Baadhi ya wadau walia kuwa utawaminya watumiaji wa takwimu Tanzania.

Dar es Salaam. Serikali inakusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 yatakayoshuhudia kufutwa kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu na kuanzisha cha Mtakwimu Mkuu na utoaji wa adhabu kali kwa yeyote atayepotosha au kukosoa takwimu rasmi kuwa siyo sahihi.

Katika marekebisho hayo yaliyopo katika 
Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya mwaka 2018 uliochapishwa katika tovuti ya Bunge, Serikali imependekeza kuanzisha kifungu cha 24A kinachodhibiti usambazaji wa taarifa rasmi za takwimu kabla ya kupitishwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS).

Kifungu hicho kilichopo katika sehemu ya sita ya muswada huo unaoonyesha ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Juni 29 2018, kinaeleza kuwa yeyote aliyethibitishwa na NBS kuchakata taarifa za takwimu rasmi anatakiwa kupatiwa kibali rasmi kabla ya kuzitoa takwimu hizo kwa umma.

Pia, Serikali katika kifungu cha 24(2) inapendekeza kumzuia mtu yeyote kutoa au kusambaza kwa umma taarifa zozote ambazo zimelenga kukanusha, kupotosha au kubatilisha takwimu rasmi.

“Yeyote atakayechapisha au kusababisha kuchapisha au atawasilisha takwimu zozote rasmi au taarifa za takwimu rasmi kinyume na matakwa ya sheria hii atakuwa ametenda kosa na atatakiwa kupewa adhabu ya faini isiyopungua Sh10 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja,” inasomeka sehemu ya muswada huo.

Katika maelezo ya sababu na madhumuni ya marekebisho hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi anasema  kuwa sheria ya sasa haina masharti yanayomtaka mtu kupata idhini ya NBS kabla ya kusambaza taarifa rasmi za takwimu.

Marekebisho mengine ya jumla yanayopendekezwa kufanywa katika sheria hiyo ya takwimu ni kufuta cheo cha Mkurugenzi Mkuu na badala yake kuweka cheo cha Mtakwimu Mkuu.

“Lengo la marekebisho haya ni kuongeza matumizi ya cheo sahihi kitakachoonesha kuwa kiongozi huyu ni mkuu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu na mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya takwimu,” inasomeka sehemu ya maelezo ya muswada huo.

Iwapo Bunge litapitisha mapendekezo ya maboresho ya sheria hiyo yanayochambuliwa na Kamati ya Katiba na Sheria kwa sasa, miongoni mwa watakaoguswa zaidi ni watafiti na wanahabari wa habari za takwimu (Data Journalists) na uchunguzi ambao baadhi ya kazi zao za kiuchunguzi huusisha uchambuzi wa takwimu za Serikali.

Kwa takriban miaka mitatu sasa wadau wa masuala ya takwimu na habari wamekuwa wakikosoa utekelezaji wa sheria hiyo ya takwimu wakieleza kuwa inaminya uhuru wa vyombo vya habari na watafiti kufanya kazi zao.

Jana baadhi ya wadau akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe walikosoa mapendekezo hayo wakieleza kuwa yamelenga kuminya uhuru wa watafiti na wanahabari nchini.

“Mabadiliko ya sheria ya takwimu ambayo yanaanza kujadiliwa na Kamati ya Bunge (ya kina @allysalehznz) leo yana lengo la kudhibiti uhuru wa kufanya tafiti, kusambaza tafiti na kutafsiri tafiti zinazotolewa na Serikali. Ni mwendelezo wa kuwa na jamii isiyohoji lolote,” aliandika Zitto katika ukurasa wake wa Twitter.

Licha ya maboresho hayo kupingwa na baadhi ya wadau, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa amenukuliwa na gazeti la Mwananchi kuwa “dhamira ya Serikali ni kupata usahihi na kwamba hakuna tatizo lolote katika utoaji wa taarifa.”

Mchengerwa amesema “kwa sasa ukiingia katika mitandao mbalimbali utakutana na takwimu zinazotolewa na nyingine watu wengine hawajafanya utafiti au si sahihi.”


Related Post