Rais Samia akemea ukabila kwa viongozi wa Serikali
- Awataka viongozi kuchapa kazi na kutokusingizia ukabila pale wanapowajibishwa.
- Asema hatoangalia kabila la mtu wakati wa uteuzi.
- Awataka viongozi kutokuwa miungu watu katika maeneo yao ya kazi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali wanaodai kuwa wanawajibishwa kutokana na makabila yao akisisitiza kuwa utendaji kazi wake hauzingatii kabila la mtu yeyote.
Amesema sumu hiyo ya ukabila imeanza kuenea katika uongozi wake na inapaswa kukemewa kama alivyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akiwaapisha viongozi walioteuliwa hivi karibuni Jijini Dodoma ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sofia Mjema, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Omar Makungu na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mustafa Siyani.
“Ninataka muangalie takwimu labda miezi sita ya kipindi hicho tulitumbua wangapi na mimi miezi sita hii nimetumbua wangapi, angalieni ambao walifanya makosa nikawatoa ni makabila mangapi, siangalii kabila ninaangalia kama unafanya kazi yako ipasavyo,” amesema Rais.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema yeye amelelewa katika misingi isiyofuata ukabila na kule anakotoka Zanzibar, wanafahamiana kwa majina ya maeneo na wala siyo makabila.
Amesema watu wanafanya makosa na wakigundulika na kuwajibishwa wanasema “nimewajibishwa kwa sababu wa kabila fulani”.
Rais Samia amesema yeye binafsi hana kabila na endapo ataulizwa kabila lake, jibu lake ni “Mzanzibari na hivyo hapangi kazi kutokana na makabila ya watu bali anaangalia sifa za mtu aliyechaguliwa.
“Uwe Mmakonde, uwe mnani, uwe mnani, ukikosea kwenye kazi mimi na wewe wala sitakufumbia jicho,” amesema Rais Samia akisema Mwalimu Nyerere amewafundisha kufanya kazi kwa kutokuangalia makabila.
Kufuatia hali hiyo, Rais Samia amewaagiza viongozi wa namna hiyo kuacha “kusambaza sumu” na badala yake waende kufanya kazi.
Kwa viongozi walioapishwa leo, Rais Samia amewataka wakafanye kazi pasi kujihusisha na vitendo vya rushwa wala kuwa miungu watu katika maeneo yao ya kazi.
“Mko kule kutumika watu na sio watu wawatumikie nyie,” amesema Rais Samia akiwasisitiza viongozi walioapishwa kusimamia kazi walizopelekwa kuzifanya.
Latest