Bajeti ya Tanzania mwaka 2023-24 yaongezeka hadi Sh44.39 trilioni
- Imeongezeka kwa Sh 2.84 trilioni sawa na asilimia 7.
- Theluthi mbili ya bajeti kutumika kwenye matumizi ya kawaida.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kukusanya na kutumia Sh44.39 trilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24, ikiwa ni ongezeko la Sh2.89 trilioni sawa na asilimia 7 kutoka bajeti inayoishia Juni mwaka huu huku zaidi ya theluthi mbili ikitumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Katika mwaka wa fedha wa fedha 2021/22 unaoishia mwezi huu yaani Juni 30, Serikali ilikadiria kukusanya na kutumia Sh41.5 trilioni.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba, amewaeleza wabunge kuwa kati ya fedha wanazopendekeza katika mwaka ujao wa fedha, Sh30.31 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 68 ya bajeti yote huku matumizi ya maendeleo yakitarajiwa kuwa Sh14.08 trilioni.
“Kati ya kiasi hicho Sh 12.77 trilioni ni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu, Sh10.88 trilioni kwa ajili ya mishahara ikiwemo nyongeza ya mshahara, upandishaji wa madaraja na ajira mpya,” amesema Dk Mwigulu.
Katika fedha hizo za matumizi Sh1.14 trilioni ni ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya kugharamia elimu msingi na sekondari bila ada pamoja na mikopo ya wanafunzi elimu ya juu na Sh5.52 trilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Hata hivyo, kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kuanzia Julai 2023 ni sawa na asilimia 31.7 ya bajeti yote iliyosomwa bungeni leo.
Soma zaidi
-
Pato la mtu Tanzania laongezeka kwa zaidi ya Sh135,000 mwaka 2022
- Deni la Serikali Tanzania laongezeka hadi Sh79.1 trilioni
- Wizara zitakazotumia bajeti kubwa mwaka 2023 – 24 Tanzania
Fedha zitatoka wapi?
Kati ya fedha hizo mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh30.23 trilioni sawa na asilimia 68 ya bajeti yote na washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh5.46 trilioni sawa na asilimia 12.3 ya bajeti.
Aidha,Serikali inatarajia kukopa mikopo ya kibiashara yenye thamani ya Sh7.54 trilioni kutoka soko la ndani na nje kwa ajili ya kulipa hati fungani na kugharamia miradi ya maendeleo.