Wizara zitakazotumia bajeti kubwa mwaka 2023 – 24 Tanzania
- Ipo Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Tamisemi
- Kiasi kikubwa kitatumika kwenye matumizi ya kawaida ikiwepo mishahara na kulipa madeni
Dar es Salaam, Zimesalia siku mbili tu Watanzania na wafuatiliaji wa masuala yanayojiri nchini kufahamu bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24 na mgawanyo wake kwenye matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.
Hii ni baada ya wizara zote 25 zilizopo nchini Tanzania kumaliza kuwasilisha bajeti zao ambapo zipo zilizopata mafungu makubwa zaidi na baadhi zimepata bajeti kiduchu tu.
Makala hii inaangazia wizara zitakazotumia bajeti kubwa katika mwaka ujao wa fedha yaani 2023/24 katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai Mosi 2023.
5. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeshika nafasi ya tano baada ya kuidhinishiwa bajeti ya Sh2.98 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 ambayo imeongezeka Sh2.7 trilioni iliyopitishwa mwaka 2022/23.
Hadi kufikia Aprili 2023 wizara hii ilikuwa imepokea Sh2.2 trilioni sawa na asilimia 82.8 ya Bajeti iliyoidhinishwa na kuwa miongoni mwa wizara zilizopokea fedha zao kwa wakati
Hata hivyo bajeti hiyo ya mwaka ujao ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kabisa kwa wizara hiyo ndani ya miaka minne iliyopita.
Kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya mwaka ujao Sh222 bilioni ya bajeti yote zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
4. Wizara ya Nishati
Namba nne imeenda kwa Wizara ya Nishati ambayo ina jukumu kubwa la kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji pamoja na ya kawaida.
Kwa mwaka 2023/24 wizara hii imeidhinishiwa kutumia Sh3,04 trilioni ikilinganishwa na Sh2.91 trilioni iliyotengwa 2022/23.
Baadhi ya vipaumbele vitakavyotekelezwa ni pamoja na kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, kuimarisha upatikanaji wa nishati vijijini na kwenye vitongoji pamoja na kuendeleza shughuli za mafuta na gesi nchini.
Hata hivyo, hadi kufikia Aprili 2023 wizara ilipokea jumla ya Shilingi trilioni 1.78 sawa na asilimia 61.2 ya bajeti iliyoidhinishwa.
Aidha, Bajeti hiyo itasomwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba kwani wizara yake ndiyo inadhamana ya kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.
3. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi nayo ni miongoni mwa wizara zilizoidhinishiwa fedha nyingi kwa ajili ya matumizi yake mwaka 2023/24 yaani Sh3.5 trilioni.
Kati ya fedha hizo Sh1.4 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi huku uchukuzi ikipata Sh2.08 trilioni sawa na theluthi mbili au asilimia 66 ya bajeti yote ya wizara hiyo.
Fedha hizo za uchukuzi zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya usafiri wa majini na nchi kavu.
2. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
Wizara ya pili itakayotumia kiasi kikubwa cha fedha ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo imeidhinishiwa Sh9.1 trilioni.
Kati ya fedha zinazoombwa, Sh5.6 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara na matumizi mengineyo.
Waziri wa Tamisemi Angela Kairuki aliliambia Bunge kuwa baadhi ya mipango itakayotekeleza na wizara yake mwaka 2023/24 ni pamoja na kufanya ukaguzi, ufuatiliaji, na tathmini kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali, taasisi na miradi katika ngazi ya mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Soma zaidi:
Bajeti ya Tamisemi yapaa kwa Sh336 bilioni
Bajeti Wizara ya Madini yaongezeka, miradi ya maendeleo ikisuasua
ACT Wazalendo waibua hoja nzito bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 2023-24
1. Wizara ya Fedha na Mipango
Kwa mara nyingine Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo imeidhinishiwa kiasi kikubwa kuliko wizara zote ambapo itatumia Sh15.9 trilioni sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.
Bajeti ya wizara hii imekuwa ikiongezeka kwa miaka mitano mfululizo ambapo hadi kufikia bajeti ya mwaka 2023/24 imeongezeka jumla ya Sh3.99 trilioni kulinganisha na ile ya mwaka 2019/20 ambayo ni Sh11.94 trilioni.
Kati ya kiasi hicho cha fedha, Sh15.3 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kiasi kilichobaki ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika kulipa deni la Serikali ambalo linaongezeka kila mwaka.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni jijini Dodoma alibainisha kuwa Sh10.48 trilioni sawa na asilimia 64.8 ya bajeti ya wizara yake zitatumika kulipa deni la Serikali.
Waziri Mwigulu amebainisha kuwa kwa mwaka 2023/24 wizara hiyo itajikita katika vipaumbele nane ikiwemo kutafuta na kukusanya mapato ya shilingi Sh40.8 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali, kufanya tafiti, pamja na tathmini na mapitio mbalimbali ya kitaalamu kuhusu mifumo ya usimamizi wa mipango, uchumi na bajeti ya Serikali.
Latest



