Deni la Serikali Tanzania laongezeka hadi Sh79.1 trilioni
- Ni sawa na ongezeko la asilimia 13.9.
- Miradi ya maendeleo yachangia ongezeko kubwa la deni hilo.
Dar es Salaam. Deni la Serikali nchini Tanzania limeongezeka hadi kufikia Sh79.1 trilioni Aprili 2023 kutoka Sh69.4 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2022 kutokana kupokelewa kwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ongezeko hilo ni sawa na Sh9.7 trilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja sawa na asilimia 13.9 ongezeko hilo la deni la Serikali limepungua kidogo kutoka kutoka kasi ya asilimia 14.4 ilyoripotiwa mwaka uliopita.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge leo Juni 15, 2023 kuwa kati ya deni hilo la Serikali, Sh51.12 trilioni au takriban theluthi mbili za deni lote ni deni la nje huku deni la ndani likiwa ni Sh27.93 trilioni.
“Ongezeko la deni limetokana na kuwepo kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya,” amesema Mwigulu jijini Dodoma.
Soma zaidi
-
Wizara zitakazotumia bajeti kubwa mwaka 2023 – 24 Tanzania
-
Wizara tano zenye bajeti ndogo mwaka 2023-24
Katika hotuba ya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 mwaka jana Waziri Mwigulu alibainisha kuwa hadi Aprili 2021, deni la Serikali lilikuwa Sh69.44 trilioni. Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa Sh47.07 na deni la ndani Sh22.37trilioni.
Hata hivyo, Kwa mujibu wa Nchemba taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Disemba 2022, inaonesha kuwa deni la Serikali bado ni himilivu na viashiria vya deni viko katika viwango vinavyokubalika kimataifa katika vipindi vya muda mfupi mda wa kati pamoja na muda mrefu.
Kwa nyakati tofauti kumekuwa na ukosoaji mkali miongoni mwa wadau wa maendeleo nchini juu ya kuongezeka kwa kasi kwa deni hilo huku Serikali ikiendelea kusisitiza kuwa ni himilifu na inakopa kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya Watanzania.
Latest



