Pato la mtu Tanzania laongezeka kwa zaidi ya Sh135,000 mwaka 2022
- Ongezeko hilo limeifanya Tanzania iendelee kuwa nchi ya kipato cha kati kiwango cha chini.
- Ni baada ya kuongezeka kwa Sh 13.9 trilioni kwenye pato la mwaka 2021.
Dar es Salaam. Wastani wa pato la taifa kwa mtu kwa mwaka nchini Tanzania limeongezeka kwa Sh135,642 ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia Sh2.84 milioni mwaka 2022, kiwango kinachoendelea kuifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya uchumi wa kati wa ngazi ya chini.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wastani wa pato la mtu (GDP per capita) kwa mwaka 2022 lilifikia Sh2,844,641 kutoka wastani wa Sh2,708,999 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 5.
Katika hotuba yake ya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/24 bungeni Dodoma leo (Juni 15, 2023) Pato ghafi la Taifa kwa bei za mwaka husika lilikuwa Dola za Marekani bilioni 77.6 sawa na Sh170.3 trilioni.
Kiwango hicho cha pato ghafi la Taifa ama GDP kwa kimombo ni kikubwa kuliko Dola za Marekani bilioni 69.94 sawa na Sh156.4 trilioni zilizorekodiwa mwaka 2021.
Wastani wa pato la mtu kwa mwaka hupatikana kwa kugawanya pato ghafi la Taifa na idadi ya watu katika eneo husika.
Dk Nchemba amesema Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inabainisha kuwa idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa 59,851,347 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu 57,724,380 mwaka 2021 hivyo kufanya pato la taifa kwa mtu kufikia Sh2.84 milioni.
“Kiasi hicho ni sawa na dola za Marekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani 1,173.3 mwaka 2021. Hali hii inaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini,” amesema Dk Nchemba.
Soma zaidi
-
Deni la Serikali Tanzania laongezeka hadi Sh79.1 trilioni
-
Wizara zitakazotumia bajeti kubwa mwaka 2023 – 24 Tanzania
- Wizara tano zenye bajeti ndogo mwaka 2023-24
Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika ndani ya miaka miwili baada ya kuathiriwa vibaya na athari na Uviko-19 na vita ya Urusi dhidi ya Ukraine zilizoathiri biashara ya kimataifa hususan mnyororo wa thamani katika masuala ya uchukuzi.
Licha ya uchumi wa Tanzania kukua bado kumekuwa na malalamiko kwa wananchi kuwa ukuaji huo hauakisi hali halisi mifukoni mwao.
Sehemu kubwa ya sekta zinazokua kwa kasi ni zile zinazojumuisha watu wachache tofauti na sekta kama kilimo ambacho kinajumuisha zaidi ya theluthi ya nguvu kazi nchini.
Mfano, katika hotuba yake ya leo, Dk Nchemba amesema sekta zilizokua kwa kasi zaidi mwaka 2022 zilijumuisha sanaa na burudani iliyokua kwa asilimia 19, madini (asilimia 10.9), fedha na bima (asilimia 9.2), malazi na huduma ya chakula, (asilimia 9) na umeme iliyokua kwa asilimia 7.6.
Hata hivyo, takwimu za leo hazikuweka bayana kasi ya ukuaji wa sekta nyingine kama viwanda na kilimo vinavyoajiri idadi kubwa ya watu Tanzania.
Latest



