Namna bajeti 2023-24 itakavyozipa ahueni startups Tanzania

June 16, 2023 11:34 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Tozo za SDL kushushwa kutoka asilimia 4 hadi asilimia 3.5.
  • Kima cha chini kujisajili na VAT chaongezwa hadi Sh200 milioni, hatua itakayotoa ahueni kwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni changa. 

Dar es Salaam. Kampuni changa zinazochipukia maarufu kama ‘Startups’ ni  miongoni mwa makundi yatakayonufaika zaidi na mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali mwaka 2023/24 baada ya kupunguza baadhi ya vikwazo vya kufanya biashara vikiwamo vya kikodi.

Katika mapendekezo ya bajeti hiyo inayoanza Julai mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba aliwaeleza wabunge kuwa Serikali inapendekeza kupunguza kiwango cha tozo ya Ufundi Stadi (SDL) kutoka asilimia 4 hadi asilimia 3.5. 

SDL yashushwa

SDL ni moja ya kodi zinazohusiana na mishahara ambazo zimekuwa zikiongeza maumivu ya gharama za uendeshaji kwa kampuni ndogo na kati zisizokuwa na mitaji ya kutosha. 

Mfano, startup yenye bajeti ya mishahara (wage bill) ya Sh10 milioni kwa mwezi inatakiwa kutoa fedha tozo za SDL ya Sh400,000. Kutokana na mapendezo hayo mapya, kampuni hiyo kuanzia Julai itatakiwa kulipia Sh350,000, ikiwa ni ahueni kidogo kuliko ilivyo sasa.

“Lengo la marekebisho haya ni kuwapunguzia waajiri gharama za uendeshaji wa shughuli zao na kutimiza azma ya kupunguza tozo hizi hatua kwa hatua bila kuathiri mapato ya Serikali kwa kiasi kikubwa,” alisema Dk Nchemba. 

Hatua hiyo, Dk Nchemba alisema itapunguza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh58.9 bilioni.

Kwa sasa startups zenye wafanyakazi chini ya 10 hazichangii tozo ya SDL ili kuzipunguzia ahueni.


Soma zaidi


Kima cha chini usajili VAT kuwa Sh200 milioni

Bajeti hiyo itakayojadiliwa na kupitishwa na Bunge kabla ya Juni kuisha pia imetoa ahueni nyingine kwa startups baada ya kupendekeza kuongeza mara mbili kima cha usajili kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kinachotakiwa kwa mfanyabiashara kusajiliwa.

Katika mapendekezo hayo, Dk Nchemba alisema Serikali inapendekeza kima hicho kiongezeke kutoka Sh100 milioni za sasa hadi Sh200 milioni na kiwango kitaendelea kuongezeka hadi kufikia Sh500 milioni ili kuepusha athari za kimapato zinazoweza kujitokeza. 

Lengo la hatua hiyo, Dk Nchemba aliwaambia wabunge jijini Dodoma kuwa ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa Kodi ya Ongezeko la Thamani na kuchochea ulipaji kodi wa hiari.

“Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh75.3 bilioni kwa kuwa walipakodi wenye mauzo ghafi kati ya milioni 100 hadi milioni 200 ni wengi lakini wamekuwa na madai zaidi kuliko kiasi kinacholipwa kutokana na udanganyifu. 

“Hivyo, walipakodi hawa wataacha kudai Serikali kodi itokanayo na manunuzi yao, sambamba na kupunguza gharama za usimamizi,” alisema. 

Mtaalamu wa masuala ya uhasibu na biashara, Doreen Audax amesema uamuzi huo utakuwa ahueni kwa kampuni ndogo kwa kuwa VAT inaongeza gharama za kuendesha biashara kwa kuwa na wataalamu wa kodi na uhasibu na ina vihatarishi vingi vitokanavyo na kutokutii sheria na taratibu. 

“Ukiwa umesajiliwa VAT unatakiwa kuwa na Mhasibu mwenye CPA au uipe kazi kampuni ya uhasibu na kodi kukufanyia kazi hiyo. Hivyo, startups nyingi hasa zenye mauzo ya Sh200 milioni zitanufaika kwa kuwa zina mitaji midogo na hazina wahasibu au wataalamu wa kodi,” amesema Audax. 

Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasili bungeni kwa ajili ya kusoma bajeti ya Serikali Mwaka 2023/24. PichalWizara ya Fedha

Tozo ya laini ya simu kwa siku yafutwa

Katika kuchochea watu kutumia huduma za fedha kidijitali, Serikali imependekeza kufuta tozo kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji ili kuchochea matumizi ya kielektroniki katika miamala mbalimbali.

Hatua hiyo, iwapo itafanikiwa kama Serikali inavyopanga itaenda kusaidia kampuni changa zinazotoa huduma kwa kupokea malipo mtandaoni kupata wateja zaidi kuliko ilivyo sasa. 

Kwa sasa baadhi ya wateja wanahofia kulipia mtandaoni kutokana na msululu wa gharama za kufanikiwa miamala (transaction fees) ambazo zinajumuisha ada ya mtoa huduma na kodi mbalimbali za Serikali. 

Kuzorota kwa kasi ya Watanzania kuingia kwa wingi kutumia malipo ya mtandaoni kumekuwa ni mwiba katika ukuaji wa bishara za wajasiriamali wa mtandaoni nchini. 

Kusamehe ulipaji ada na kuwasilisha nyaraka nje ya muda

Katika mapendekezo hayo, Dk Nchemba Serikali inatarajia kufanya marekebisho ya sheria ya kampuni kutoa msamaha wa ulipaji wa ada na kuwasilisha nyaraka nje ya muda. 

“Notisi hiyo pia itaainisha kampuni zitakazohuisha taarifa zake kwenye mfumo ndani ya kipindi cha miezi 12 ambapo zitasamehewa asilimia 50 ya ada ya kuwasilisha nyaraka nje ya muda,” alisema Dk Nchemba.

Marekebisho hayo yatazihusu kampuni ambazo zilisajiliwa kabla ya mfumo wa Online Registration System (ORS) kuanza kutumika ambayo ni mwaka 2017.

Miamala ya ununuzi hisa mpya, uhamishaji kutotozwa kodi

Miongoni mwa changamoto kubwa zinazozikabili startups Tanzania ni ugumu wa kupata mitaji kutokana na uchache wa wawekezaji. 

Katika kutatua hilo, Serikali inapendekeza kurekebisha Sheria ya Kodi ya Mapato ili miamala ya utoaji wa hisa mpya na uhamishaji wa miliki ya kampuni unaofanyika ndani ya nchi isitozwe kodi ya mapato.

“Lengo ni kuvutia uwekezaji nchini na kutoa ufafanuzi,” alisema Dk Nchemba.

Kampuni ndogo na za kati ni miongoni mwa taasisi zinazohaha kuvutia wawekezaji ili kuongeza mitaji na kukuza biashara zao.

/
No matches found for this filter
31 May, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
31 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
31 May, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
AKILI UNDE INAVYOIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

AKILI UNDE INAVYOIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

Nukta TV

WAFAHAMU 'THE BIG FIVE' WA AFRIKA

WAFAHAMU 'THE BIG FIVE' WA AFRIKA

Nukta TV

HIVI NDIVYO UNAWEZA KUSAFISHA MENO YAKO

HIVI NDIVYO UNAWEZA KUSAFISHA MENO YAKO

Nukta TV