Microsoft yaachana rasmi na ‘Internet Explorer’
- Ni programu tafutishi ya kwanza kwa mamilioni ya watumiaji wa kompyuta.
- Ni kutokana na kuongezeka kwa ushindani wa soko la programu tafutishi.
- Imefungwa rasmi mara baada ya miaka 25.
Dar es salaam. Baada ya kupita miaka 27, kampuni ya teknolojia ya Marekani inayotengeneza vifaa vya kielektroniki imeachana rasmi na matumizi ya kivinjari chake maarufu na cha kwanza cha “nternet Explorer” tangu wiki iliyopita.
Microsoft imeachana na programu hiyo tafutishi ya vitu mtandaoni tangu Juni 15 mwaka huu.
Kivinjari cha Internet explorer ambacho huenda ni cha kwanza kwa mamilioni ya watumiaji wa kompyuta ulimwenguni. Kinafahamika pia kam “IE”,au “MSIE” kilianzishwa mwaka 1995 kama sehemu ya programu endeshi ya kompyuta (Window 95) ambapo tangu wakati huo mpaka mwaka 2013 kampuni hiyo ilikuwa imetoa matoleo 11 ya kivinjari hicho.
Kivinjari hicho kilifika kilele cha mafanikio katika miaka ya 2000 ambapo mwaka 2003 ndiyo ilikuwa programu tafutishi iliyotumika zaidi ulimwenguni kwa asilimia 95, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kutokana na programu hiyo kuwa ya lazima katika kompyuta zilizotengenezwa na kampuni ya Microsoft.
Ushindani katika soko la programu tafutishi ulianza kuchomoza mwaka 2002 mara baada ya kuanzishwa kwa kivinjari cha Mozilla Firefox mwaka 2000 na Google Chrome mwaka 2008.
Soko la Internet explorer lilishuka mpaka chini ya asilimia 50 mwaka 2010 na mwaka 2012 Google Chrome ilichukua usukani na kuwa ndiyo Programu tafutishi inayotumiwa zaidi duniani.
Zinazohuziana:
- Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Ushindani ulizidi kuongezeka zaidi ambapo mwaka 2022 watumiaji wa Internet Explorer walikuwa chini ya asilimia moja kwa mujibu wa kampuni ya Statcounter.
Mwaka 2015 Microsoft walitengeneza programu tafutishi ya Edge ambayo ilitajwa kuwa mbadala wa Internet Explorer lakini bado haifanyi vizuri sokoni kwani ina asilimia nne tu ya watumiaji duniani kote ndiyo wanaitumia.
Chrome ndiyo programu tafutishi inayopendwa na huku ikimiliki asilimia 64.9 ya soko ikifuatiwa na Safari (asilimia 19) na Edge yenye asilimia 4 ya watumiaji ulimwenguni kote.
Baadhi ya watu waliowahi kutumia kivichari akiwemo Charles Joseph mkazi wa jijini Dar es salaam amesema uamuzi wa kufuta programu hiyo tafutishi ulikuwa sahihi kwa sababu ilikuwa haina ufanisi mzuri wa utendaji ukilinganisha na programu nyingine.
“Haiko rahisi kutumia ukilinganisha na programu tafutishi nyingine, ugumu wake umetokana na kuwa na taarifa nyingi ambazo mara nyingi huwa haziendani na matakwa ya mtumiaji wake hivyo anaamini Microsoft kuachana nayo kutawapa nafasi ya kutafuta iliyo bora na rafiki kwa mtumiaji wa kawaida,” amesema Joseph.
Latest
