Microsoft kuboresha mikutano ya mtandaoni

November 5, 2021 11:38 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaanzisha programu ya avatar kwa watumiaji wa jukwaa lake la vikao na mikutano.
  • Itamuwezesha kushiriki kikao kwa kutumia mdoli ambao unafanana na yeye.
  • Pia iko katika mpango wa kuanzisha vizimba vya mtandaoni kwa ajili ya vikao.

Dar es Salaam. Kuna sababu nyingi za kwanini watu huzima kamera wakati wa vikao vya mtandaoni. 

Huenda ni kutokana na ubora wa kamera, mazingira waliyopo na wakati mwingine, wapo ambao hutundika koti” nikimaanisha huingia kwenye kikao huku wakiendelea na kazi nyingine.

Kukabiliana na baadhi ya sababu hizo, kampuni ya teknolojia ya Microsoft imeibuka na mfumo ambao utamwezesha mtu kuchagua kutumia midoli (avatar) wakati wa kikao cha video za mtandaoni.

Teknolojia hiyo itamwezesha mtu kushiriki kikao kwa kutumia mdoli ambao unafanana na yeye.

Hilo linawezekana kufanyika kupitia jukwaa la vikao vya mtandaoni ambalo linatengenezwa na kampuni ya Microsoft la Microsoft Teams.

Maboresho yanayofanywa na Microsoft ni mwendelezo wa kuwekeza katika mfumo mpya wa utendaji kazi kwa njia ya mtandao ambao ulichochewa na janga la Corona (Uviko-19).

Microsoft imeitambulisha programu hiyo ya avatar ambayo itaanza kufanya kazi katika kipindi cha  nusu ya kwanza ya mwaka 2022 ambapo mtu akiingia katika vikao au mikutano ya mtandaoni kwa kutumia Microsoft Teams atakuwa na uwezo wa kuchagua kuingia kama yeye au avatar yake ndiyo ionekane.

Mfumo mpya utaruhusu watumiaji kutengeneza vyumba vya kufikirika. Picha| The Verge.

Siyo jambo geni kwa Microsoft kuboresha jukwaa la Teams kwani mwaka jana iliinzisha muundo wa “Together Mode” ambao uliupa mkutano wa mtandaoni muonekano wa kikao au unaweza kuita “conference”.

Kupitia “Together Mode”, mtu anaonekana wakati wa kikao kUanzia sehemu ya kichwa na kuishia mabegani na hivyo kuhifadhi faragha yake na eneo alilopo.

Sehemu ya mwili inayobaki itafunikwa na kiti kufanya mtu kuonekana kama yupo kwenye kikao kabisa.

Mbali na “Together Mode”, Microsoft iliongeza mfumo wa “Dynamic View” ambao unamruhusu mtumiaji wa Microsoft Teams kufanya mawasilisho kwa njia ya makundi.

Awali mawasilisho yalikuwa yanafanyika na mtu kuonekana anachangia ni hadi aanze kuongea tu.

Dynamic View iliwapatia watumiaji muonekano tofauti wanakikundi ambao wanafanya wasilisho ili kikundi kijulikane na kionekane tofauti na wasikilizaji wengine.

Hadi sasa, Microsoft Teams inaruhusu watumiaji 1,000 hadi 20,000 kujiunga na kikao au mkutano kwa wakati mmoja.

Microsoft pia inafanya kazi ya kuwezesha watumiaji wa teams kutengeneza maeneo/vizimba vya mtandaoni (virtual spaces) ambavyo vitakuwa na muonekano kama wa ofisi zao kwa ajili ya kuboresha vikao vya mtandano.

Maboresho ya Microsoft yanaenda sambamba na kampuni ya Meta, awali Facebook ambayo pia inatengeneza majukwaa ya mfumo kama unaojengwa na Microsoft.

Ushindani utakuwaje?, wacha tutulie tuone hali inavyoenda.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW