Kasi ya mfumuko wa bei yang’ang’ania kiwango cha Julai 2023
- Mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishi Agosti 2023 ulikuwa asilimia 3.3.
- Kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula kwatajwa kama sababu.
- Kasi ya mfumuko wa bei yapungua Kenya na Uganda.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia Agosti 2023 imebaki asilimia 3.3 sawa na kiwango cha mwaka unaoishia Julai mwaka huu.
Hali hiyo imechangiwa zaidi na kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula.
“Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2023 kuwa sawa na ule ulioishia mwezi Julai, 2023 umechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2023,” imeeleza taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Septemba 9, 2023 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Kusalia kwa kiwango kile kile cha kasi ya mfumuko wa bei huenda kukatoa ahueni kwa walaji ambao walikuwa wakilazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kumudu gharama za msingi za bidhaa na huduma kama chakula.
Itakumbukwa kuwa kiwango cha kasi ya mfumuko wa bei kilichoripotiwa mwezi Julai ndio ndio kiwango kidogo zaidi kilichowahi kurekodiwa ndani ya mwaka mmoja.
Mara ya mwisho kasi ya mfumuko wa bei wa taifa wa asilimia 3.3 iliripotiwa katika mwaka ulioishia Aprili na Mei, 2021 na tangu wakati huo mfumuko wa bei ulikuwa ukipanda na kushuka lakini haukuwahi kushuka zaidi ya kiwango hicho.
Soma zaidi
-
Mambo yatakayozisadia nchi za Afrika kuongeza mapato ya kodi
-
Mambo ya kuzingatia unapoanza ‘freelancing
-
Mambo ya kuzingatia unapoanza ‘freelancing’ 2
Bidhaa zilizochangia mfumuko wa bei kusalia pale pale
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti, 2023 ni pamoja na ngano, mchele, mahindi, unga wa mahindi, karanga, mihogo, ndizi za kupika, maharage, na kunde.
Hata hivyo, mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za chakula umeonekana kupanda ikilinganishwa na mwaka ulioishia Julai, 2023 zikiwemo nguo za wanaume, viatu vya wanawake, viatu vya watoto, nishati ya gesi, nishati ya mkaa , nishati ya kuni, na samani za nyumbani.
Aidha NBS imeeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Agosti, 2023 nao umepungua hadi asilimia 5.6 kutoka asilimia 6.1 kwa mwaka ulioishia Julai, 2023.
Kwa upande wa mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Agosti, 2023 umeongezeka hadi asilimia 2.4 kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka ulioishia Julai, 2023.
Ahueni hadi nchi jirani
Wakati mfumuko wa bei ukisalia kiwango kilekile nchini, Kenya na Uganda nazo zimepata ahueni baada ya mfumuko huo kushuka katika nchi zao.
Nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti, 2023 umepungua hadi asilimia 6.7 kutoka asilimia 7.3 kwa mwaka ulioishia Julai, 2023.
Huenda kushuka kwa mfumuko wa bei nchini humo kumechangiwa na hatua ilizochukua Serikali ya Kenya ya kuondoa baadhi ya kodi baada ya shinikizo la wananchi na baadhi ya viongozi wa upinzani akiwemo Raila Odinga.
Kwa mujibu wa NBS, nchini Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti, 2023 umepungua hadi asilimia 3.5 kutoka asilimia 3.9 kwa mwaka ulioishia Julai, 2023.
Latest