Simulizi ya hali livyokuwa mahakamani Lissu akihukumiwa
- Katikati mwa jiji la Dar es Salaam ilikuwa ni mshike mshike na ulinzi mkali.
Dar es Salaam. Kwa yeyote aliyekuwa anaingia katikati mwa Jiji la Dar es Salaam leo hapana shaka alishuhudia ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi uliokuwa umeimarishwa hususan Barabara ya Sokoine ilipo Mahakama Kuu ya Tanzania.
Tangu alfajiri ya Novemba 6 saa chache tu kabla ya hukumu ya kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu kuanza, askari wa jeshi hilo wenye silaha walikuwa wametanga eneo hilo wengine wakiwa kwenye farasi na magari ya washawasha.
Kadri muda ulivyokuwa unaenda ndivyo ulinzia ulivyokuwa ukiimarishwa katika eneo la Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambako kesi iliyomhusu ilikuwa ikiendelea.
Lissu aliletwa na maofisa wa Jeshi la Magereza majira ya Saa 2:20 asubuhi na kuingizwa moja kwa moja ndani ya eneo la mahakama chini ya ulinzi mkali kiasi cha waandishi kushindwa kupata hata picha ya tukio hilo.
Baada ya kiongozi huyo kuingizwa ndani ya jengo la mahakama, polisi waliendelea kuimarisha kwa kumkagua na kuzuia baadhi ya watu waliokuwa wakiingia mahakamani hapo. Sehemu kubwa ya watu wakiwemo wafuasi wa Chadema walizuia kuingia.
Hali hiyo ya ulinzi mkali ilisababisha magari kuganda kwenye foleni kwa takribani dakika 10 kutokana na mpangilio wa ulinzi na shughuli za kiusalama zilizokuwa zikiendelea barabarani kuelekea mahakamani.
Sehemu kubwa ya waliokuwepo eneo la mahakama ni waandishi wa habari ambao wachache walibahatika kupatiwa fursa ya kuingia chumba cha mahakama. Polisi waliruhusu mwandishi mmoja tu kila chombo na si wote walifanikiwa kuingia katika chumba ambacho hukumu hiyo inayosomwa licha ya baadhi kufika hapo tangu Saa 11 alfajiri.
Kwa baadhi ya wananchi waliotokea maeneo ya Mbezi, pamoja na wafuasi na baadhi ya viongozi wa Chadema waliowasili mahakamani baada ya kesi kuanza, nao walibaki nje ya jengo la mahakama.
Walielezwa kuwa hakukuwa na nafasi ya kutosha ndani ya mahakama kwa kuwa tayari kulikuwa kumejaa.
Sehemu kubwa ya wafuasi walifurushwa na polisi waondoke eneo hilo warejee makwao wakiwemo waliokuwa wameambatana na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Majira ya saa 2:40 asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro aliwasili nje ya mahakama na kueleza kuwa hali ni shwari licha ya kuwa siku ilikuwa bado haijaisha.
Katika kipindi chote nilichokuwepo mahakamani, hali ya ulinzi iliendelea kuwa imara, huku wananchi wakawaida, wanafunzi na wafanyabiashara wa maji, karanga na pweza wakiendelea na heka heka zao katika eneo hilo.
Lakini, takribani kila baada ya nusu saa, magari ya polisi yalikuwa yakifika katika eneo la mahakama.
Askari waliokuwa ndani ya magari hayo wengine wakivalia nguo vitambaa vyeusi vilivyoziba sehemu kubwa za sura zao walishuka na kufanya ukaguzi wa hali ya usalama katika maeneo mbalimbali, kisha kuondoka.
Hali hiyo iliendelea licha ya kuwepo kwa askari wengine waliokuwa wakilinda maeneo ya ndani ya mahakama, nje ya jengo pamoja na kando ya barabara.
Baada ya kesi kumalizika na Lissu kuhukumiwa miaka minne kwa kosa dogo mbadala ya uchoche, baadhi ya wanawake waliotoka nje ya jengo la mahakama ikiwemo wafuasi wa Chadema walikuwa wakifuta machozi kwa mikono huku wengine wakimshukuru Mungu na walivyoanza kuimba walizuliwa kufanya hivyo eneo la mahakama.
Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu kifungo cha miaka minne jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la uchochezi, uamuzi unaomwingiza kiongozi huyo katika historia ya kukutwa na jinai.
Awali Lissu alishtakiwa kwa kosa la uhaini kutokana na maneno aliyatamka April 3, 2025 jijini Dar es Salaam kwa kuazimia kuhamasisha umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2025 na kuonyesha hia hiyo kwa kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lissu alikana mashtaka hayo.
Lissu alitoka mahakamani hapo na kupelekwa jela na gari aina ya Toyota Land Cruiser LX nyeupe iliyokuwa na vioo vilivyozuia kuonekana ndani majira ya Saa 7:45 mchana na kisha kusindikizwa na msafara wa magari ya magereza na polisi.