Hesabu, bado mfupa mgumu kwa watahiniwa darasa la saba 2023

November 24, 2023 5:57 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ufaulu washuka kwa asilimia 4.4 kulinganisha na ule wa mwaka 2022
  • Zaidi ya nusu ya watahiniwa wafeli.
  • Ufaulu wa masomo mengine wapanda na kushuka.

Dar es Salaam. Huenda Serikali na wadau wa elimu nchini wakawa na kibarua cha kutafuta muarobaini wa kuongeza ufaulu wa somo la Hesabu  mara baada ya ufaulu wa somo hilo kushuka kwa asilimia 4.4 huku zaidi ya nusu ya watahiniwa wakifeli katika mtihani wa darasa la saba 2023.

Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed leo Novemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam yanaonesha ufaulu umeshuka kutoka asilimia 52 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 48.8 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Necta ufaulu wa masomo hayo unapimwa katika daraja A, B na C.

Jumla ya watahiniwa milioni 1.3 wa darasa la saba walisajiliwa kufanya mtihani wa Taifa uliofanyika Septemba 13 na 14 mwaka huu, wasichana wakiwa 742,690 (sawa na asilimia 53).

Kati ya hao, wavulana wamefaulu sana somo hilo kwa asilimia 52.4 ukilinganisha na asilimia 45.6 ya wasichana.

Hata hivyo, Dk.Mohamed amesema licha ya kushuka kwa ufaulu wa somo hilo idadi ya wanafunzi waliopata A katika somo hilo imeongezeka huku wale waliopata daraja E ikipungua.

“Idadi Ya waliopata grade(daraja) A imeongezeka kwa asilimia 0.33 …Hisabati ndio somo lenye watahiniwa wachache zaidi waliopata grade(daraja)  E yani asilimia 0.15 grade(daraja) E ni alama ya sifuri mpaka 10,” amesema Dk. Mohamed.


Soma zaidi:Necta yawafutia watahiniwa 31 matokeo kwa udanganyifu


Zaidi ya nusu wafeli

Aidha, matokeo hayo yameonesha kuwa watahiniwa waliofeli somo hilo kwa mwaka huu ni asilimia 51 idadi iliyoongezeka kwa asilimia 4.4 kutoka watahiniwa 46.7 waliofeli somo hilo mwaka 2022.

Idadi hiyo ni sawa na kusema nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Hesabu walifeli somo hilo.

Hiyo inamaanisha katika kila watahiniwa 10, watano wamefeli somo hilo linaloumiza vichwa wanafunzi wengi nchini.

Wakati idadi ya watahiniwa wa darasa la saba wakifeli kwa kupata alama D na E watahiniwa waliopata Daraja A nao wameongezeka kiduchu kwa asilimia 0.33.

Mwaka 2022 waliopata A walikuwa 43,405 ambapo iwa mwaka 2023 wameongezeka hadi 48,145.


Soma zaidi : Ufaulu matokeo ya darasa la saba waongezeka kiduchu


Ufaulu wa masomo mengine wapanda na kushuka

Ufaulu wa masomo mengine yaliyofanywa na wanafunzi wa darasa la saba umependa na kushuka jambo linalotoa nafasi kwa wanafunzi na walimu kuongeza jitihada zaidi katika masomo hayo.

Kwa upande wa somo la kiingereza ufaulu umepanda kwa  asilimia 4.9 na kufikia asilimia 34.35 huku somo la kiswahili likishuka hadi asilimia 87.91 ukilinganisha na matokeo ya somo hilo kwa mwaka 2022.

Aidha, masomo ya Sayansi na Teknolojia,  Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi pamoja na Uraia na Maadili yamepanda kwa  asilimia 74, 77.4 na asilimia 82 mtawalia ukilinganisha ya yale ya mwaka jana.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW