Jaji Warioba awananga wanaopuuzia tahadhari za Uviko-19
- Asema wapo viongozi na wanasiasa wanaohubiri wasiotenda.
- Asema tabia hiyo inawachanganya wananchi kuhusu ugonjwa huo.
- Awataka wanahabari kuongeza elimu ya Uviko-19.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba amewataka wanasiasa na viongozi wa Serikali kutenda wanayohubiri kuhusu tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19) ili kutokuwachanganya wananchi wa kawaida kuhusu ugonjwa huo.
ahadhari hizo ambazo zimekuwa zikishauriwa na wataalam wa afya ni pamoja kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, kukaa kwa kuachiana nafasi angalau mita moja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Njia nyingine ya uhakika ya kujikinga na Uviko-19 ni kuchanja chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
Jaji Warioba, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, amesema baadhi ya viongozi na wanasiasa wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari hizo lakini wao wenyewe hawachukui wanapokuwa katika shughuli zao.
“Unamwambia mtu avae barakoa, asiende kwenye mikusanyiko lakini wewe kiongozi unawakusanya wananchi wanabanana hawana barakoa, sasa maana yake nini?,” alihoji Jaji Warioba Septemba 10, 2021 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2020 zilizoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Amesema tabia hiyo siyo nzuri kwa sababu viongozi wanatakiwa kuwa mfano bora kwa wanaowaongoza ili kuepusha upotoshaji na maswali yasiyo na msingi kuhusu afya zao.
“Pamoja na maelezo ya watalaam kuna conspiracy theories (nadharia zisizo za kweli) nyingi sana kiasi ambacho mwananchi wa kawaida hajui kipi afuate,” amesema Jaji Warioba aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Kiongozi huyo mstaafu ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya MCT amesema kama tahadhari dhidi ya Uviko-19 zitaendelea kupuuzwa kama wanavyoshauri wataalam wa afya, uchumi wa nchi utaendelea kudhoofika na kuathiri maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia Septemba 7, 2021, Tanzania ilikuwa imerekodi visa 1,367 vya Corona na vifo 50 vilivyotokana na maradhi hayo.
Licha ya Serikali na wataalamu wa afya kuhimiza watu kufuata tahadhari ni wachache sana wameonekana kufuata miongozo hiyo ya kujikinga na Uviko-19.
Warioba amesema vyombo vya habari vimefanya kazi nzuri kuwahabarisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 lakini vinatakiwa pia kuwakumbusha viongozi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kivitendo.
“Sijasikia mkiwakumbusha viongozi kwamba watende yale wanayosema kwa sababu kupitia wao wananchi watajifunza haraka zaidi. Tukifanya hivyo itasaidia (kupunguza maambukizi ya Uviko-19),” amesema kiongozi huyo mstaafu.
Julai mwaka huu, Tanzania ilipokea dozi zaidi ya milioni moja za chanjo ya Corona aina ya Johnson & Johnson ikiwa ni msaada kupitia mpango wa usambazaji chanjo wa Covax ulioratibiwa na Umoja wa Afrika (AU).
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya hadi kufikia hadi Agosti 28, 2021, watu 304,603 walikuwa wamepatiwa chanjo. Kiwango hicho cha waliopatiwa chanjo ni sawa na asilimia 30 au takriban theluthi ya dozi zote zilizoingizwa Tanzania.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).
Latest
