Majaliwa: Endeleeni kuchukua tahadhari dhidi ya Corona

July 21, 2021 8:35 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema ugonjwa huo upo nchini japokuwa kuna wagonjwa wachache. 
  • Ashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima.
  • Asema chanjo iko nchini, hiari kwa wananchi kuchanja.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakumbusha na kuwasisitiza wananchi wa Tanzania waendelee kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa Corona (Uviko-19).

Majaliwa ameyasema hayo leo Julai 21, 2021 wakati wa ibada ya Sikukuu ya Eid Al Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Mtoro jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa ugonjwa huo upo nchini japokuwa kuna wagonjwa wachache. 

“Tuendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka na sabuni na tukikosa maji tutumie vitakasa mikono. Tuvae barakoa zilizothibitishwa na mamlaka zetu,” amesema Majaliwa

Mtendaji huyo mkuu wa Serikali amesema ni vema kwa sasa wananchi wakajiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na wazingatie kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Amesema wananchi wanatakiwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara kulingana na afya zao pamoja na kuweka safi mazingira yanayowazunguka huku akiwasihi wazingatie lishe bora.

“Kwa wale wenye umri mkubwa na wenye uzito uliopitiliza na wenye magonjwa sugu kama moyo, pumu, kisukari na figo wanapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kujikinga na ugonjwa huu,” amesema.

Wananchi wametakiwa kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili za mafua makali, maumivu ya koo, kichwa kuuma, kupumua kwa shida, kukosa hamu ya kula na kupoteza uwezo wa kunusa harufu mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu chanjo ya ugonjwa huo, Waziri Mkuu amesema chanjo hiyo ipo tayari nchini, mwananchi yoyote anayetaka kuchanjwa akachanje kwa ajili ya kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo.

“Tumesema kuchanja ni hiari, hivyo kama unataka kuchanja nenda mahali zilipo. Kama unaona umuhimu mwakani kwenda Hijja, una watoto wanasoma nje ya nchi na hairuhusiwi kwenda mpaka uwe umechanjwa basi fursa ipo hapa hapa usiangaike kwenda nje,” amesema.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW