Watu zaidi ya 81,000 hufa kila mwaka kwa kung’atwa na nyoka: WHO

September 17, 2021 6:23 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Waathirika wakubwa ni watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo na watoto.
  • Takriban watu milioni 5.4 hung’atwa na nyoka kila mwaka duniani.
  • Matibabu salama na yenye ufanisi yatasaidia kupunguza athari hizo.

Dar es Salaam. Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linasema watu 81,000 hadi 137,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na athari zinazosababishwa na kung’atwa na nyoka wenye sumu.

Waathirika wakubwa ni watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo na watoto huku maeneo yaliyoathirika na kuwa hatarini zaidi ni Afrika, Asia na Amerika ya Kusini hasa vijijini.

Kwa mujibu wa WHO, barani Asia watu wapatao milioni 2 hudhurika na sumu ya nyoka kila mwaka wakati Afrika watu 435,000 hadi 580,000 huhitaji matibabu kila mwaka baada ya kung’atwa na nyoka.

Ingawa idadi kamili ya waliong’atwa na nyoka hadi sasa haijulikani lakini makadirio yanaonyesha kuwa takriban watu milioni 5.4 hung’atwa na nyoka kila mwaka huku milioni 2.7 kati yao hung’atwa na nyoka wenye sumu kali ambao husababisha athari mbaya kwa mamilioni ya maisha ya watu na wengi wao wakiwa masikini. 

Mbali ya vifo vya watu hadi 137,000 kila mwaka, kung’atwa na nyoka pia kumewaacha mamilioni ya watu na vilema vya maisha. 

WHO inasema kung’atwa na nyoka mwenye sumu kali kunaweza kusababisha kupooza ambako kunaweza kumzuia mtu kupumua, kumsababishia maradhi ya kutokwa na damu, matatizo ya figo yasiyoweza kutibika na kuharibu mishipa na kusababisha ulemavu wa maisha na kukatwa viungo. 

Shirika hilo limeongeza kuwa kung’atwa na nyoka ni moja ya magonjwa yasiyoambukizwa ambayo athari zake ni kubwa na mbaya kuliko inavyodhaniwa.  

Ili kupunguza idadi ya vifo na ulemavu utokanao na kung’atwa na nyoka, WHO imesema ni lazima kuziwezesha na kuzishirikisha jamii, pili kuhakikisha kuna matibabu salama na yenye ufanisi, tatu kuimarisha mifumo ya afya na nne kuongeza ushirika, uratibu na rasilimali za kupambana na zahma hii. 

Pia shirika hilo limezindua jukwaa maalum mtandaoni kwa lengo la kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu hatari ya kung’atwa na nyoka wenye sumu na wapi waliko nyoka hao hatari zaidi duniani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW