Bidhaa za tumbaku zinavyopukutisha maisha ya watu duniani
- Watu milioni 8 hufariki dunia kwa kutumia bidhaa za tumbaku.
- Huchangia katika ukataji wa miti na uchafuzi wa hewa.
- WHO yashauri mshikamano katika kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mikakati thabiti inahitajika kuokoa maisha ya watu milioni 8 kila mwaka wanaofariki dunia kutokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.
WHO katika ripoti yake kuhusu tumbaku iliyotolewa Mei 29, 2022 imeeleza kuwa tumbaku siyo tu inagharimu maisha ya watu bali ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.
Sekta ya tumbaku husababisha uharibifu wa miti milioni 600, hekta 200,000 za ardhi, tani bilioni 22 za maji na kuzalisha tani milioni 84 za hewa ya ukaa.
Ripoti hiyo imeanisha kuwa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa tumbaku pamoja na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unachangia asilimia moja ya tano ya hewa ya ukaa, ambayo inasababisha kuongezeka kwa joto duniani.
“Bidhaa za tumbaku ni bidhaa zilizojaa zaidi kwenye sayari, zina zaidi ya kemikali za sumu 7,000, ambazo huingia kwenye mazingira yetu zinapotupwa,” amesema Dk Ruediger Krech, Mkurugenzi wa Kukuza Afya katika WHO.
Dk, Ruediger ameongeza kuwa vichujio vya sigara trilioni 4.5 huchafua bahari zetu, mito, njia za mijini, mbuga, udongo na fukwe kila mwaka.
Bidhaa kama vile sigara, tumbaku isiyo na moshi na sigara za kielektroniki pia huongeza mkusanyiko wa uchafuzi wa mazingira, bidhaa hizo hutengeneza uchafu wa plastiki wenye madhara kwenye mazingira.
Hali hiyo imejitokeza wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupinga matumizi ya tumbaku.
Soma zaidi
- Tumbaku: Rafiki wa mashaka anayeiweka tanania njia panda.
- Tumbaku inavyohatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni 2 Tanzania.
Namna gani tumbaku huathiri mazingira?
Mchakato wa kuzalisha tumbaku hutumia kuni nyingi ambapo mti mmoja hutumika kutengeneza takribani sigara 300.
Madhara mengine ni upotevu wa rasilimali maji, ripoti hiyo imefafanua kuwa katika shughuli za uzalishaji wa bidhaa za tumbaku, lita 3.5 za maji hutumika kutengeneza kipande kimoja cha sigara.
Pia viwanda vya kuzalisha bidhaa za tumbaku huzalisha hewa ya ukaa kwa wingi hasa utengenezaji wa sigara kuanzia uzalishaji mpaka usambazaji.

Hatua za kuchukua kupunguza matumizi ya tumbaku
WHO, kwenye ripoti iliyochapishwa mwaka 2021 iliyoitwa “ripoti ya ulimwengu kwenye janga la tumbaku” imependekeza hatua sita za kupunguza janga hili la matumizi ya tumbaku ikiwemo kutazama upya matumizi ya tumbaku na sera za kuzuia kuongezeka kwa matumizi yake.
Hatua nyingine ni kulinda jamii na moshi utokanao na tumbaku, kutoa msaada wa kuacha matumizi ya tumbaku pamoja na kutoa tahadhari juu ya madhara ya tumbaku.
Kuweka sheria kwenye matangazo ya bidhaa za tumbaku na udhamini wa bidhaa hizo na kuongeza kodi kwenye zao la tumbaku ni hatua zinazopendekezwa na WHO.
Nchi zenye uchumi wa chini na uchumi wa kati zinashauriwa zaidi kufuata hatua hizi ili kuondokana na athari za tumbaku kwani tafiti za WHO zinasema asilimia 80 ya watuamiaji wa tumbaku wanatoka kwenye nchi zenye uchumi wa chini na wa kati.
Latest
