Muheza ilivyoshinda vikwazo utoaji chanjo ya Uviko-19
- Imechanja asilimia 72.1 ya dozi 2,000 ilizopokea.
- Elimu na kuwafuata watu vijijini kumesaidia muamko wa kuchanja.
- Serikali yawataka watu kuchukua tahadhari hata baada ya kupata chanjo.
Tanga. Kama ni utoaji chanjo ya Corona (Uviko-19) basi Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga basi umepiga hatua kubwa baada ya kufanikiwa kuchanja zaidi ya nusu ya chanjo ilizopokea mwezi uliopita.
Hadi kufikia September 17, 2021, Halmashauri hiyo imefanikiwa kutoa dozi za chanjo 1,453 sawa asilimia 72.1 ya dozi zote 2,000 ilizopokea.
Muheza imefanikiwa kupiga ikilinganishwa na utoaji chanjo katika Mkoa wa Tanga ambapo Mganga Mkuu wa mkoa Dk Jonathan Budenu, akitoa takwimu za chanjo Septemba 22 alisema walikuwa na lengo ni kuchanja walengwa 139, 000 lakini wameweza kufikia watu 10,939.
Mwenendo huo unadhihirisha wazi kuwa, Muheza ikongeza hamasa kwa watu wake inaweza kukamilisha zoezi hilo ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo aikua rahisi kufikia kiwango hicho licha ya ni kidogo ikilinganishwa na idadi ya watu waliopo wilayani humo wanaofikia 204,461 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk Habi Mwasangala ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa mafanikio hayo yamepatikana baada ya jitihada mbalimbali zilizofanyika kuwafikia watu kutoka maeneo mbalimbali hasa vijijini ambapo ni mbali na vituo vya kutolea chanjo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, awali halmashauri hiyo ilikuwa na vituo vitatu vya kutolea chanjo ya Uviko-19: Hospitali ya Wilaya Muheza, Kituo cha Afya Ubwari na Mkuzi.
Mbali na utaratibu wa kutembelea kituo cha afya kupata chanjo, halmashauri hiyo ilianzisha utaratibu wa wataalamu wa afya kufuata watu vijijini ambapo iliwasaidia kufikia watu wengi zaidi.
Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza. Picha | Gift Mijoe
Dk Mwasangala amesema wameanzisha utaratibu mpya unaohusisha kutembelea maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kama jitihada mojawapo za utoaji chanjo wilayani humo.
“Tumeingia kwenye mpango mwingine. Tumeona kuna maeneo ambayo yana idadi kubwa ya watu kama maeneo ya stendi, masokoni na maeneo mengine, haya tumeyawekea ratiba maalum kila siku,” Dk Mwasangala ameiambia Nukta.
Kwa mujibu wa Dk Mwasangala amesema utaratibu huo utawahitaji wahudumu kuweka kambi katika maeneo hayo kuanzia asubuhi mpaka jioni kwa ajili ya huduma ya utoaji chanjo.
Licha ya kuwafuata watu katika maeneo yao, elimu zaidi inahitajika kwa watu kuhusu faida za kuchanjwa chanjo hiyo ili kuondoa dhana potofu ambazo watu wanazo kwenye jamii ikiwemo hofu.
“Mimi nasubiri nione wenzangu waliochanja kama hawatapata madhara basi na mimi nitachanja. Nisije nikachanja nikapata madhara kama wanayosema ya damu kuganda,” amesema Safina Shemhina, mkazi wa halmashauri hiyo.
Wakati Safina akisubiri kusikia matokeo kutoka kwa wengine, Amina Yusuph anawakilisha kundi kubwa la watu waliochanja huku akihimiza watu kwenda kuchanja.
“Sikushawishiwa na mtu yeyote kwenda kuchanja, nilipoona mkuu wetu wa wilaya ameenda kuchanja nilikuwa nyuma yake maana najua ugonjwa huu ni hatari,” amesema Amina akionekana mwenye kujiamini.
Hata hivyo pamoja na zoezi hilo la utoaji chanjo kuendelea Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Nassib Mmbagga amesema wanaendelea kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.
Tahadhari hizo ni pamoja kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na kuepuka mikuanyiko isiyo ya lazima.
Zaidi amewaasa watu waendelee kujitokeza kwa wingi katika zoezi la utoaji chanjo linaloendelea mkoani humo.
Hivi karibuni Serikali ya Tanzania ilitoa maagizo kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa chanjo dhidi ya Uviko-19 ili kuhakikisha kuwa chanjo za ugonjwa huo ziishe mapema.
Dozi za chanjo zilizoingizwa nchini kutoka nchini Marekani kupitia mpango wa chanjo wa COVAX ni milioni 1.058 ambapo hadi kufikia Septemba 15 zaidi ya nusu ya chanjo hizo bado zilikuwa hazijatumika.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuchanja ni hiari.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest
