KCB yaongeza muda wafanyabiashara kurejesha mikopo Mwanza

October 22, 2021 6:08 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Wafanyabiashara ambao ni wateja wa KCB benki wakiwa kwenye semina ya kujengewa uwezo na kupatiwa elimu ya masuala ya kibenki na bidhaa zinazozalishwa nabenk hiyo ikiwemo mikopo. Picha|Mariam John.


  • Ni baada ya biashara zao kuathiriwa na janga la Uviko-19.
  • Wanatakiwa kurudisha kati ya miezi sita na mwaka mmoja.
  • Yasitisha kutoa mikopo kwa sasa.

Mwanza. Huenda wafanyabiashara jijini Mwanza wakapunguza makali ya athari za Corona (Uviko-19) katika shughuli zao, baada ya benki ya biashara ya Kenya (KCB) kuwaongezea muda wa mwaka mmoja kurejesha mikopo yao.

Zaidi ya wafanyabiashara 500 wadogo na wa kati walikuwa wamekopa katika benki hiyo kabla ya ugonjwa huo kuingia Tanzania Machi 2020.

Benki hiyo kwa sasa imewapatia wateja wao muda wa kulipa kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja na kupunguza kiwango cha marejesho.

Mfanyabiashara wa nafaka jijini hapa, Jovina Temu ni ambaye husambaza bidhaa hiyo mashuleni anasema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hakuweza kufanya biashara kutokana na shule kufungwa.

“Katika kipindi chote ambacho shule zilifungwa biashara ilisimama wateja walipungua sana, niliamua kwenda KCB kuwaelezea nashukru walinipa mawazo na walinipunguzia kiwango cha marejesho na  kuniongezea muda wa kulipa,” amesema Temu.

Meneja wa Tawi la KCB Mwanza, Emmanuel Mzava amekiri kuwa katika kipindi hicho zipo sekta ambazo ziliathirika zaidi ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii na biashara.

Amesema sekta hizi ziliathirika kutokana na janga la corona ambalo lilisababisha shughuli zao kuyumba hali iliyosababisha kushindwa kurejesha mikopo yao kwa wakati 

“Baada ya kitendo hicho benki tuliona ni vema tuongeze muda wa kulipa kuanzia miezi sita na wengine miezi 12, lakini pia kutokana na kuepuka msongaman (katika matawi yetu) , benki ilianzisha huduma mbalimbali  za kidijitali,” amesema Mzava.

Uanzishaji wa huduma za kidijitali umesaidia kuboresha utendaji wa benki na kuwawezesha watumiaji wa huduma za kifedha kuzipata kwa urahisi na haraka katika simu zao.

“Baada ya hali hiyo benki ilisitisha kwa muda kutoa mkopo, sasa ni takribani  mwaka mzima hatujatoa mikopo badala yake tumeongeza muda wa wateja wetu kurejesha mikopo yao na wale ambao wanamaliza na wanahitaji mikopo mingine benki inawaangalia,” anesema Mkuu wa kitengo cha biashara ndogo na rejareja wa KCB , Abdul Juma.

Kila mwaka, KCB huendesha semina ya wafanyabishara, lengo ni kuwapa elimu inayohusiana na masuala ya kibenki na bidhaa zinazozalishwa na benki hiyo ikiwemo mikopo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW