Pambazuko jipya: Wafanyabiashara bidhaa za utamaduni, sanaa Zanzibar
- Waanza kupata wateja tena baada ya kuathiriwa na Uviko-19.
- Waeleza Uviko-19 ilivyopukutisha mifuko yao.
- Serikali yasema itashirikiana nao kuimarisha biashara zao.
Zanzibar. Miaka mitatu iliyopita ilikuwa ni kawaida kuingia katika duka hili na kukuta watu wanapishana mlangoni huyu akiingia na huyu akitoka kwa ajili ya kujipatia bidhaa.
Ni duka la kituo cha utamaduni Zanzibar kilichopo Mtaa wa Stone Town katika Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani hapa. Duka hili ni moja ya sehemu chache ambazo zinajishughulisha na uuzaji wa bidhaa za utamaduni visiwani Zanzibar.
Duka hilo pia linatoa fursa kwa wafanyabiashara mbalimbali kuuza bidhaa za utamaduni ili kujipatia kipato wakati wakijifunza masuala mbalimbali ya utamaduni.
Bidhaa zinazopatikana katika duka hilo ni pamoja na picha zilizochorwa kwenye karatasi na mbao, bangili, mikufu, mikoba, shanga, foronya za mito, madaftari na vifaa vya kuhifadhia bidhaa ambavyo vimekwa nakshi na urembo wa utamaduni wa Kitanzania.
Kulipia kodi na gharama za kuendesha biashara haikuwa kitu kigumu kwani mbali na biashara walizokuwa wakifanya, walikuwepo wafadhili waliokuwa wakifanya kazi na kituo hiki.
Yote hayo yalikuwa yakifanyika miaka mitatu iliyopita kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Uviko-19) kuingia Tanzania Machi 2020. Miezi michache baadaye duka hili lilifungwa kama hatua za kuwakinga wafanyabiashara na wanunuzi dhidi ya ugonjwa huo.
Baadhi ya bidhaa zinazouzwa katika duka la kituo cha Utamaduni Zanzibar. Picha| Rodgers George.
Mambo yalibadilika ghafla. Wafanyabiashara wa duka hili wakapoteza ajira kwa muda na mipango ya kukuza utamaduni nayo ikafifia.
“Tulikuwa hatuna elimu ya kutosha kuhusu Corona hivyo tuliichukulia kwa uzito na moja kwa moja tukachukua hatua ya kufunga kituo,” anasema mmiliki wa kituo hicho, Hamad Mbarouk Hamad.
Duka hilo ni miongoni mwa biashara mbalimbali ambazo zinazotoa huduma za utalii ambazo ziliathiriwa na Uviko-19 duniani, jambo lililosababisha watu kupoteza ajira na mapato ya sekta ya utalii kushuka.
Baada ya takriban mwaka mmoja wa kutoa huduma, kituo hicho kilifunguliwa tena Juni 2020 na kuanza kutoa huduma kama awali, baada ya Serikali kufanikiwa kukabiliana na Uviko-19 ikiwemo utoaji wa chanjo na kulegezwa kwa masharti ya kimataifa ikiwemo safari za watalii wa kimataifa.
Biashara yarejea mdogo mdogo
Kwa sasa, shughuli katika kituo hicho zimerejea kama kawaida lakini hazijachanganya kama zamani.
“Walau wageni sasa wanakuja na wafanyabiashara wanafanya mauzo,” anasema Hamad akiweka wazi kuwa kituo hicho ni tegemeo kwa vijana zaidi ya 100 ambao wanajihusisha na kutengeneza, kufundisha na kuelimisha kuhusu kazi mbalimbali za sanaa.
Baadhi ya wafanyabiashara katika kituo hicho waliozungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wanaeleza kuwa kwa sasa wana matumaini makubwa kuendelea kufaidika na kazi za sanaa na utamaduni kwa sababu janga la Uviko-19 linadhibitiwa.
Mjasirimali wa kutengenza vitabu na sabuni kutoka kituo hicho, Fatma Yusuph Ally anasema kwa sasa ameshusha bei ya bidhaa zake ili kuvutia wateja wakati akiangalia namna ya kuimarisha biashara yake ambayo aliifunga wakati wa Uviko-19.
“Zamani nilikuwa nauza sabuni kwa Sh5,000 lakini sasa nawauzia hadi Sh3,500,” anasema Fatma ambaye kwa sasa anawauzia watu wa kawaida wakati akisubiri watalii wa kimataifa ambao ni wateja wake kurejea visiwani humo.
Mjasiriamali Alphonce Lazaro akiwa nje ya duka lake la kuuzia bidhaa za sanaa. Picha| Rodgers George.
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO), limesema sekta ya utalii duniani itaimarika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022, huku Afrika, sekta hiyo ikitarajiwa kuimarika kwa asilimia 73.
Kampeni ya utoaji chanjo ya Uviko-19 katika mataifa mbalimbali inaweza kuchangia sekta ya utalii kurejea katika hali nzuri, kutokana na kupunguzwa kwa masharti ya safari za kimataifa.
Wajasiriamali wa foronya katika kituo hicho, Masha Idiame na Miza Haji Hassan wameiambia Nukta Habari kuwa licha ya Uviko-19 kuathiri biashara zao lakini bado wana matumaini makubwa kuendelea kufaidika na shughuli hizo.
Akina mama hao wanasema mauzo yao yalishuka kutoka Sh800,000 kwa siku hadi kutokuuza kabisa. Licha ya hayo, bado walilazimika kuendelea kulipa hela ya kodi ya duka lao.
“Hivi unapotuona hapa juzi ndiyo tumemaliza kulipa deni la kodi ilikuwa kila tunachouza tunaenda kulipa deni,” anasema Idiame.
Hata hivyo, baada ya kulipa deni lao, kina mama hao wanaamini kuwa pesa watakayoanza kuipata itaanza kuwanufaisha.
“Walau sasa hivi wanaingia watu kuangalia bidhaa na wengine wananunua japo kwa uchache,” anasema Hassan.

Serikali yawakumbuka wajasiriamali
Licha ya kuwa shughuli za biashara za utamaduni na sanaa kuanza kurejea tena baada ya Zanzibar kuanza kupokea watalii ambao ndiyo wateja wakuu wa bidhaa hizo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongeza matangazo ya utalii ili kuvutia wageni wengi.
Afisa Utalii wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Said Soud Said anasema Serikali imeruhusu ndege za moja kwa moja zinazotoka nchi mbalimbali ikiwemo Ufaransa na Urusi ili kutokuwapatia watalii vikwazo vya kufika visiwani humo ikiwemo kutua katika nchi ambazo bado zina masharti makali dhidi ya Uviko-19.
Serikali pia imetoa mafunzo kwa wajasiriamali juu ya kujikinga ugonjwa huo ili kuendelea kuwa salama na pia kuwahudumia vizuri wageni kwa huduma na bidhaa wanazouza.
“Wajasiriamali wamepewa maelekezo ya njia za kujikinga na ugonjwa wa Corona. Pia kuna masomo yametolewa kwa wanaotembeza watalii tuliwafundisha jinsi gani ya kuhudumia wageni,” anasema Said.
Mafunzo hayo yamesaidia wakazi wa Zanzibar kuendelea kuchukua tahadhari ambazo hazifukuzi wala kuwapa watalii wasiwasi ikiwemo matumizi ya barakoa, kunawa mikono, kutumia vitakasa na kupata chanjo.
“Wanavyotuona tunaishi hivi kidogo inawapa moyo kwani tunajikinga lakini siyo kama ilivyo kwenye nchi zao,” anasema mtaalam huyo.
Kwa upande wa kodi, Said anasema Serikali ilitoa ruhusa ya wajasiriamali kuomba kulipa kodi kidogo kidogo ili kuwapunguzia makali ya Uviko-19.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest
