Utafanya nini kama unategemewa kuikomboa sayari inayoteketea?
- Ni katika filamu ya Dune inayomhusu kijana Paul Atreides.
- Licha ya kukosa miraba sita, Paul anabaki tumaini la sayari inayoteketea.
- Mapenzi, kisasi na usaliti ni sehemu ya filamu hii ya kufikirika.
Dar es Salaam. Inasemekana kila ndoto ina maana yake. Kule kukimbizwa na viumbe usiowajua, kuona sehemu ambazo hazieleweki na hata saa zingine kuelea angani, kote kuna maana yake.
Paul Atreides, ndoto yake ilikuwa ni mwanadada Chani na alikuwa akimwita kwenda kuwasaidia huko kwenye sayari yao ambayo inateketea.
Ingekuwa rahisi kwa Paul kuipotezea ndoto hiyo lakini haikuwa rahisi kwa sababu ilikuwa ni ya kujirudia rudia.
Mbaya zaidi, asingeweza kuisukumia ndoto hiyo chini ya uvungu kwani baadhi ya ndoto alizoziota zimetokea hivyo kwa ile hatari ambayo Chani alikuwa akimwambia Paul ndotoni, bila shaka inatarajiwa kutokea.
Unaweza kudhani Paul ni baunsa wa kutisha sana kiasi cha kuchaguliwa kuikomboa sayari ambayo ipo karibu kuteketezwa lakini wala, ni kimbao mbao tu kama mimi hapa.
Wakati familia yake ikiwa imezungukwa na walinzi wenye miili iliyojengeka, Paul anaonekana ni goigoi asiyejua hata kusihika kisu. Hata hivyo, wahenga walisema, umdhaniaye siye kumbe ndiye.
Usiyemtarajia anaweza kuwa mtu tofauti. Picha| Games Radar.
Amani inayovurugwa
Filamu ya Dune inaanza na amani kana kwamba ni ile “happily ever after” ambayo huonekana katika filamu nyingi. Amani inavurugika baada ya sayari ya Arrakis kuvamiwa na majeshi ambayo kuua mamilioni wala siyo dhambi kwao.
Majeshi hayo yanawateketeza viumbe jamii ya Fremen ambao ndiyo wakazi wa sayari ya Arrakis.
Waarakis wanauliwa wengi na tena kwa mafungu na kufanya majeshi mengine kuungana ili kumkabili adui ambaye teknolojia yake, siyo ya nchi hii.
Hakuna kitu kinauma kama kuwa mdhaifu kwenye familia. Yaani wakati wenzio wote wana nguvu za kupambana na kujilinda, inabidi wafikirie na kukulinda na wewe kwa kuwa hauwezi kujifanyia hivyo.
Hiyo ndiyo hali anayokutana nayo Paul ambaye amezaliwa ili awe kiongozi lakini ndani yake, anahisi kuwa huo siyo wito wake.
Usaliti wa kugeuza rafiki adui, safari ya kutafuta mwito halisi wa maisha na nguvu ya huba, ni sehemu ya kinachowasilishwa na wasanii mahiri akiwemo Timothée Chalamet, Rebecca Ferguson, Dave Bautista, Zendaya na Jason Momoa katika skrini za kuangaliza filamu za Century Cinemax.
Unasubiri nini, katazame filamu ya Dune nisije nikakumalizia uhondo wote.
Latest