Safari ya furaha inayoiachia familia simanzi

September 3, 2022 5:44 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni filamu ya ‘Beast’ ambayo imetoka hivi karibuni.
  • Inamhusu baba ambaye aliandaa safari kwa ajili ya kurudisha ukaribu kati yake na bintize.
  • Safari hiyo inaingia dosari baada ya kukutana na simba mwindaji watu.

Dar es Salaam. Majukumu ya kila siku yamekuwa yakitusogeza mbali na maisha ya kijamii. 

Kwa baadhi, huenda mbali zaidi na kuwasogeza mbali na familia yaani baba kuwa mbali na mkewe na watoto,  mama kuwa mbali na watoto na mume au watoto kuwa mbali na wenzao.

Mara nyingi huanza pale vitu vinavyowaweka pamoja vinapotoweka. Kukosekana kwa muda ambao awali mlitumia kula chakula pamoja, kutokuwepo wasaa wa kutazama filamu kama ndugu na rafiki au kila mtu kushikilia la kwake na kuwasahau wenzie.

Ni hali kama hiyo inayomsababisha baba wa familia ya watu watatu yaani yeye na binti zake wawili kutafuta suluhu ya jangwa la upweke linaloikumba familia yake ambapo suluhu iliyopo ni moja. Safari.

Filamu ya ‘Beast’, inaanza na mgane ambaye adhma yake ni kurudisha ukaribu kati yake na bintize wawili. Baba huyo ambaye ni Dk Nate Samuels anaamua kuandaa safari kwa ajili yake na binti zake wawili na sehemu inayomjia kichwani ni moja tu.Mapone. 

Huko, anaamini watoto wake watapata kumbukumbu za mama yao na kujua mambo mbalimbali yanayowahusu.

Nguo zinakunjwa, mabegi yanafungwa, viatu vinavaliwa na ndege zinapandwa. Safari ya kuelekea Mapone imewadia. Wakiwa angani, wanaona mambo mengi, makundi ya wanyama, milima, mito na mengine mengi ya kuvutia.

Furaha ya kuona historia ya mama yao inawapa upweke watoto hawa lakini hawako peke yao, wapo na baba yao ambaye anafanya jitihada kubwa za kuziba pengo ambalo kamwe, haliwezi kuzibika.

Siku moja wakiwa matembezini, mambo yanakwenda pasi na walivyodhania. Wanakutana na mtu ambaye amejeruhiwa vibaya. Wanapouliza, anajibu “ni shetani”.

Kabla muda haujawapa nafasi ya kuendelea kushangaa, “shetani” ambaye alikuwa anaongelewa anaingia ndani ya picha. Ni simba ambaye ameshararua kujeruhi na kuua mamia ya wanakijiji wa Mapone.

                             

Kwa Dk Samuels anachokitaka ni kuhakikisha watoto wake wapo salama na katika kufanya hivyo, mambo hayaendi sawa na mipango. Ni nini kilitokea? Watoto walifanikiwa kuwa salama? Na dhumuni ambalo Dk Samuels alilikusudia na wanae linatimia?

Tazama filamu hii kupitia kumbi za sinema zilizo karibu na wewe huku ukiwa na uhakika wa burudani na mafunzo ya maisha.

Kutana na Idris Elba, Sharlto Copley, Iyana Halley na nguli wengine kibao katika tasnia ya filamu.

Sambamba na ‘Beast’, filamu kali zinazotarajiwa  kuingia sinema ni pamoja na ‘Woman King’ bila kusahau ‘Avatar’? Wewe unaingoja ipi? Tuachie maoni yako kupitia mitandao yetu ya kijamii (@nuktatanzania iwe Twitter, telegram, Facebook, Instagram) ili tujadili pamoja.

Tokwibona hange.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

Nukta TV

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV