Bei ya petroli, dizeli yapaa tena Novemba
- Ni baada ya kushuka kwa miezi mitatu mfululizo.
- Sh10,000 sasa itanunua lita 2.44 za petroli Dar es Salaam, kutoka lita 2.46 mwezi uliopita.
Dar es Salaam. Bei za mafuta nchini zimepanda kwa mwezi wa pili mfululizo baada ya kushuka kwa miezi mitatu mfululizo, jambo linaloacha maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto nchini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo Novemba 4, 2026 imesema bei ya rejareja ya petroli imepanda kwa Sh26 na Sh42 dizeli.
Kwa viwango hivyo vipya, lita moja ya petroli inayopitia Bandari ya Dar es Salaam itauzwa kwa Sh4,083 kutoka Sh4,057 mwezi Oktoba huku dizeli ikipanda hadi Sh4,128 kutoka Sh 4,086 mwezi ulipita.
Mafuta ya taa nayo mwezi huu yanauzwa kwa Sh4,117 kutoka Sh4,067 mwezi uliopita.Â
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa kiwango hicho cha bei ya mafuta Novemba ndiyo cha juu zaidi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kuanzia Januari 2023 hadi Oktoba 2026 kiwango hicho cha bei ya petroli, na dizeli kilikuwa kikipanda na kushuka kwa wastani wa bei ya Sh2,819 hadi Sh3,295.
Watumiaji wa vyombo vya moto walianza kuionja shubiri ya kupaa kwa bei ya mafuta mwezi Machi, 2026 baada ya vita vya Marekani, Israel na Iran.
Tangu wakati huo bei ya mafuta duniani ilipaa suala lilosababisha maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto na wananchi wa kawaida baada ya bei ya baadhi ya bidhaa muhimu pia kuongezeka.
Kwa bei hiz mpya za mafuta Dar es Salaam, Sh10,000 sasa itanunua lita 2.44 za petroli, ikilinganishwa na lita 2.46 zilizopatikana mwezi Octoba
Kwa dizeli, kiasi hicho kitamwezesha mtumiaji kupata lita 2.42 kutoka lita 2.44 zilizopatikana kwa Sh10,000 mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, ongezeko hilo la bei ya mafuta limechagizwa na kuendelea kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, ambako Tanzania hununua sehemu kubwa ya mafuta yake.
Mgogoro huo umeongeza gharama za usafirishaji na bima, hivyo kuongeza gharama za uagizaji wa mafuta.
Sanjari na kupanda kwa bei hizo, Ewura imewataka wafanyabiashara kuuza mafuta kulingana na bei elekezi huku hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo hilo.