Machinga walia kupungua biashara Mwanza

November 2, 2021 8:18 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni waliahamishiwa maeneo mapya wakitoka katikati ya jiji.
  • Wasema maeneo waliyopangiwa hayana wateja.
  • Wengine wahaha kurejesha mikopo taasisi za fedha.

Mwanza. Wakati Serikali ikiendelea na zoezi la kuwapanga wafanyabiashara wadogo (wamachinga) katika maeneo waliyotengewa,  wafanyabiashara hao wamesema bado wanakumbana na hali ngumu ya kiuchumi tangu zoezi hilo lianze kutokana na kupungua kwa biashara. 

Halmashauri ya jiji la Mwanza ilitoa maeneo ya Mchafukuoga,  Dampo la  Buhongwa,  soko la Mirongo na Mbugani kuwa ni maeneo ya wafanyabiashara hao ambapo takwimu zilizotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi zinaeleza kuwa zaidi ya machinga 12,000 walishahamia katika maeneo hayo. 

Mbali na maeneo hayo pia Halmashauri hiyo ina jumla ya masoko 17 ambayo yalikuwa yametelekezwa na wafanyabiashara ambao  walihamishia bidhaa zao barabarani lakini sasa wamerudi.

Nukta habari (www.nukta.co.tz) imetembelea eneo la dampo Buhongwa ambapo ni mwendo wa takriban dakika 45 kutoka katikati ya jijini Mwanza kujionea mwenendo wa biashara.

Wamachinga wanandelea na shughuli za kuuza bidhaa, ujenzi wa vibanda vyao na wengine wakiendelea kupangiwa maeneo. 

Baadhi ya wafanyabiashara ambao wameanza kuuza bidhaa, wanasema biashara bado haijachangamka kwa sababu wako mbali mji ambapo wateja wao bado hawajaanza kufika huko. 

Mfanyabiashara katika eneo hilo, Ashura Mohammed anasema biashara mauzo yake yameshuka sana ikilinganishwa na alivyokua akiuza bidhaa barabarani, jambo linalompa wakati mgumu wa kutunza mtaji wake.

“Tuna marejesho tunadaiwa fedha tulizokopa na biashara hatufanyi huku tulikohamishiwa  hakuchangamka kabisa,” amesema Ashura. 

Mfanyabiashara mwingine wa bidhaa za nyumbani, Shija Ndaki amesema ana wiki mbili tangu ahamie katika eneo hilo lakini hauzi kwa sababu wateja hamna tofauti analivyokuwa katikati ya jiji.

Anasema awali walikuwa wakiwafuata wateja katika maeneo husika hasa kwenye vituo vya daladala na barabarani na hivyo kurahisisha mchakato wa kuwauzia bidhaa.

“Walizoe kununua bidhaa barabarani, sasa kuna kazi ya kuwaelimisha wananchi kuwa wanatakiwa watufuate huku sokoni,” amesema Ndaki.

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula (mwenye shati la njano) akiwasikiliza wafanyabiashara wa nyanya katika soko la Buhongwa alipotembelea hivi karibuni. Picha| BMG.

 Wafanyabiashara hao wamesema shauku yao ni kuona wateja wanafika katika eneo hilo. Ili kufanikisha hilo wameomba Serikali kuimarisha miundmbinu ya barabara na usafiri wa daladala kupita katika masoko mapya.

 “Magari yapo yanayofanya safari kati ya mjini na Nyashishi kituo cha kushusha abiria kipo soko la Buhongwa ambapo ni mbali kufika hapa,  ombi letu kwa Serikali ni kuweka kituo hapa ili kurahisisha huduma,” anasema Fausitine Chilogela, mfanyabiashara wa dampo la  Buhongwa

 Vilio vya wafanyabiashara hao nikuona Serikali inaweka vituo kwenye maeneo ambayo wametengewa, katika maeneo yote hakuna maegesho ya daladala  hali inayosababisha wateja kutofika kufanya mahemezi. 

 Hulazimika kutumia bajaji au bodaboda kupeleka bidhaa sokoni jambo linalowaongezea gharama za usafiri na kupunguza faida.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema zoezi la kuwahamisha machinga limefanikiwa na sasa wapo kwenye maeneo yao wakiendelea na biashara huku wakitatua changamoto zinazoibuka katika maeneo mapya ya biashara.

“Kuhusu suala la safari  za magari na maegesho karibu na maeneo hayo linafanyiwa kazi,  muda si mrefu suala hilo litatatuliwa,” amesema Makilagi

Kauli Kama hiyo pia iliwahi kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Mhandisi Robert Gabriel ambaye aliagiza Wakala wa Barabara (Tanroads)  kushugulikia suala la maegesho huku pia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu ( Latra)  ikianzisha safari za daladala kwenye maeneo hayo. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW