Wamachinga walia migambo kukamata bidhaa zao Mwanza

April 21, 2022 6:24 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kusumbuliwa na migambo wa jiji.
  • Wasema biashara zao zinaharibiwa bila sababu za msingi.
  • Serikali kuchukua hatua zaidi kuwalinda.

Mwanza. Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel kuchukua hatua kwa migambo wa jiji la Mwanza waliohusika katika tukio la kumnyang’anya ndizi mmoja wa wafanyabiashara wadogo Buhongwa, baadhi ya machinga wamesema hatua zaidi zinahitajika kulinda biashara zao.

Hivi karibuni video fupi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha migambo wa jiji la Mwanza wakipakia ndizi za mmoja wa machinga kwa jina la Tumaini Mkono. 

Baada ya video hiyo kusambaa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Innocent Bashungwa aliutaka uongozi wa Mkoa wa Mwanza kujitathimini kwa tukio hilo.

Kutokana na maagizo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel  alichukua hatua ya kusimamisha viongozi wa mgambo pamoja na wote waliokiwepo kwenye operesheni hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa, pia alimwalika Tumaini kula naye chakula cha mchana nyumbani kwake na kumpatia kiasi cha fedha kwa ajili ya kuendeleza biashara yake.

Wakizungumza na Nukta Habari, Aprili 20, 2022, baadhi ya machinga wamesema migambo wamekuwa na tabia ya kuchukua bidhaa za wafanyabiashara wanaowakuta kwenye maeneo waliyoondolewa kisha kuzipeleka katika ofisi ya Mkurugenzi wa jiji.

Tuma Ashatu ni mfanyabiashara wa matunda amesema tabia ya migambo hiyo haijaanza sasa, imekuwepo tangu walivyohamishiwa kwenye maeneo yaliyotengwa.

“Tulikohamishiwa hakuna biashara  kinachofanyika ikifika mida ya jioni machinga wengi hufungasha bidhaa zao na kuwafuata wateja wao ambapo wanapatikana kwa wingi lakini kitendo hicho hawakipendi wanachokifanya wanakusanya bidhaa zao na kwenda kuzimwaga kwenye gari lao na kuondoka nazo,” amesema Ashatu.


Soma zaidi:


Emiriana Kazimiri, mfanyabiashara wa Mwanza amesema wanawake wengi wamelizwa na kuachwa na madeni kwenye vikundi kwa kuwa bidhaa zao zinakamatwa na kupelekwa jiji.

“Mimi mwenyewe ni mhanga wa tukio hilo bidhaa zangu za nguo zilikamatwa na nilipoenda kufuatilia sikukuta zile nguo za maana zilikuwa zimechambuliwa zote, na hata nilipoulizia sikuweza kupatiwa jibu la uhakika,” amesema Emiriana

Anasema pale mgambo anapochukua bidhaa huzipeleka jiji na ukiamua kufuatilia unaambiwa ulipe faini si chini ya Sh200,000 ya kukiuka masharti ya kufanyia biashara maeneo  ambayo hayaruhusiwi.

Anasema sio kwamba muda wote hufanya biashara eneo la Buhongwa ni mida ya jioni tu kuanzia  saa 1 ambapo watu wengi wanakuwa wanatoka makazini na eneo hilo ndiyo stendi kubwa ya mabasi lakini kwa muda huo bado wanakamata bidhaa zao.

Hali hiyo, imekuwa ikiwaweka katika wakati mgumu machinga hao huku wakiiomba Serikali kuwahakikishia usalama wa mali zao.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wafanyabiashara wadogo Mkoa wa Mwanza, Said Tembo amesema wafanyabiashara wengi wamedhurumiwa bidhaa zao.

“Madhira ni mengi kwa wafanyabiashara hao, wengi wamefanyiwa vitendo vya kinyama na kudhalilisha kiukweli hali si nzuri,” amesema Tembo.

Licha ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa hatua alizochukua kwa migambo pia ameomba kuwepo kwa ushirikishwaji kati ya viongozi wa machinga katika hatia zote wanazotaka kufanya ili kupunguza changamoto kama hizo.

“Toka zoezi la kuwapanga machinga lifanyike yapo mambo yanayofanywa na migambo ambayo ni kinyume na utu watu wanakamatiwa bidhaa zao, wanadhalilishwa na kudhurumiwa bidhaa zao pale wanapoenda kuzikomboa, tukio hilo ni mfano tu lakini yanayoendelea ni mengi kuliko hilo,” amesema Tembo. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW