Machinga wapewa saa 24 kuhamia maeneo waliyopangiwa Mwanza

October 21, 2021 1:28 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wale ambao bado wako katikati ya jiji.
  • Serikali yasema waondoke kwa hiari.
  • Oktoba 23 kuanza kampeni ya usafi katika maeneo yaliyoachwa na wamachinga.

Mwanza. Serikali mkoani Mwanza imewaagiza wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga wanaofanya biashara zao katikati ya mji (Makoroboi) kuhamia kwenye eneo lililopangwa ndani ya masaa 24.

Baadhi ya maeneo mapya yaliyotengwa kwa ajili ya machinga ni viwanja vya Mchafukuoga na Mbungani ambavyo viko katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Agizo hilo limetolewa leo Oktoba 21, 2021 baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi  Robert Gabriel kutembelea eneo la Makoroboi kwa ajili ya kujiridhisha kama machinga wanatekeleza makubaliano ya kuhamia katika maeneo waliyopangiwa.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa sababu biashara katika eneo hilo zinaendelea kama kawaida.

“Nipo hapa na timu nzima hakuna kinachoendelea na kinachofanyika, tulichokubaliana ni kinyume bado watu wapo, nitoe agizo  mwisho leo muwe mmehamia kwenye maeneo yaliyotengwa,” amesema Mhandisi Gabriel.

Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza viongozi wa machinga  kusimamia zoezi hilo ilikupisha maduka waliyoyaziba .

Zoezi la kuwahamisha wamachinga linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku Serikali ikisisitiza kuwa zoezi hilo lifanyike kwa utulivu na amani na maeneo watakayopangiwa machinga yawe na miundombinu rafiki ikiwemo vyoo.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa ametangaza kampeni ya usafi wa mazingira itakayoanza Oktoba 23 mwaka huu  ili kuweka jiji la Mwanza safi baada ya  machinga kuondolewa maeneo yasiyokuwa rasmi.

Amesema barabara zote zinatakiwa kufanyiwa usafi ili kuliweka jiji katika hali ya usafi na kwamba viongozi wote mkoani humo wasimamie mpango huo.

“Kwa siku jiji la Mwanza linazalisha tani 1,120 za takataka na kwamba asilimia 75 zinazolewa na kupelekwa kutupwa dampo,” amesema Gabriel.

Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza  Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri katika mkoa wa Mwanza kuangalia vigezo vya kampuni za kuzoa takataka zilizopo jijini humo ili kubaini ambazo hazifanyi kazi vizuri na kuziondoa.

Amesema suala la usafi kwa sasa litakuwa agenda ya kudumu ili kuliweka safi jiji hilo na kwamba kila mwananchi anao wajibu wa kuhusika  na mpango huo.

Kuhusu taa za barabara kutowaka baadhi ya maeneo jijini  Mwanza nyakati za usiku, Gabriel aliagiza mamlaka zinazohusika kurekebisha tatizo hilo kwa haraka.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW