Tanzania kuomboleza kifo cha Malkia Elizabeth II kwa siku tano
- Bendera zote nchini na kwenye ofisi za balozi kupepea nusu mlingoti.
- Rais Samia awaomba Watanzania kuungana na Waingereza kuomboleza.
Dar es salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza maombolezo ya siku tano kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II wa Uingereza kilichotokea Septemba 8 mwaka huu huko Uskochi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo maombolezo yanaanza leo hadi Septemba 14, 2022.
Katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti nchini Tanzania pamoja na kwenye ofisi zake za balozi.
“Rais Samia amewaomba Watanzania wote kuungana na wenzetu wa Uingereza katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na aliyekuwa kiongozi wao nchini humo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia ya kifalme, Malkia Elizabeth amefariki kifo cha amani akiwa na umri wa miaka 96, baada ya kutawala kwa muda wa miaka 70 na kutajwa kuwa utawala mrefu zaidi katika historia.
Anatarajia kupumzishwa katika nyumba yake ya milele huko Westminister ndani ya siku 10 baada ya kifo chake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Malkia Elizabeth II (96) wa Uingereza aliyefariki tarehe 08 Septemba, 2022 nchini Uskochi. @venusnyota
pic.twitter.com/qeYPbJnLEp— ikulu_Tanzania (@ikulumawasliano) September 9, 2022