Watendaji halmashauri ongezeni ubunifu- Majaliwa

January 24, 2022 7:02 am · Maria
Share
Tweet
Copy Link
  •  Amewataka watendaji kuanzisha miradi ili kuwezesha vikundi vinavyohitaji mikopo. 
  • Wanufaika wa mikopo watoa shukrani kwa Serikali kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji katika halmashauri zote nchini waongeze ubunifu na waanzishe miradi inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vinavyohitaji mikopo hiyo ili viweze kupata maendeleo. 

Majaliwa ametoa maagizo hayo Januari 23, 2022 wakati akikabidhi pikipiki na guta kwa kikundi cha vijana kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Hanang’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Manyara. 

Waziri Majaliwa aliwataka Watendaji hao kutafuta namna nzuri na rafiki ambayo itasaidia kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali na baadaYe kuleta matokeo chanya kwa wanufaika wa mikopo.

“Kutoa Sh20,000 ukasema umewaridhisha watu wakati mwingine anayepata siyo mlengwa, tuna walemavu, wanawake lakini pia vijana.Tuende tukabuni namna nzuri ya kutumia fedha ile asilimia 10 kwa utaratibu mzuri kuliko kusambaza pesa kidogo kidogo zisizoleta matokeo,” amesema Majaliwa.

Amesema kuwa kitendo cha kuwakusanya vijana na kuwatafutia jambo la kufanya na lenye tija ni hatua nzuri, kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza viongozi kuwa na maono ya mbali yanayoangalia Watanzania na mahitaji yao.


Zinahusiana:


Akizungumza kwa niaba ya vijana walionufaika na mkopo huo, Damian Kalist ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ ambayo ilitoa Sh385 milioni kwa vikundi 87.

“Mkopo huu ni nafuu na umetuwezesha kuondokana na mikopo kandamizi yenye riba kubwa iliyokuwa ikitolewa na baadhi ya taasisi mbalimbali za kifedha. Mikopo hii imetusaidia kutuinua kiuchumi na kutuongezea pato la familia na nchi kwa ujumla,” amesema Kalist.

Kalist amesema kuwa kupitia mikopo hiyo wameweza kupata ajira binafsi pamoja na kutoa ajira kwa vijana wengine, hivyo kuwafanya vijana kuondokana na utegemezi wa kipato.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW