Teknolojia ya umeme tayari kuwanufaisha walemavu, wazee
Afisa Mkuu Masoko Tanesco Makao Makuu, Monica Massawe akitoa elimu ya matumizi sahihi ya kifaa cha umeme tayari yaani (UMETA) kwa wananchi wa Kitongoji cha Nyamatagito kijiji cha Nyamwigura kata ya Binagi Wilayani Tarime Mkoani Mara. Picha|cleo24news
- Serikali imeagiza kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalum katika zoezi la kuunganishiwa umeme kwa kutumia vifaa hivyo ili kuwapunguzia hadha ya upatikanaji wa nishati.
- Kifaa hicho kinawapungiwa gharama kufunga mfumo wa umeme katika nyumba zao.
Dar es Salaam. Huenda watu wenye mahitaji maalum wakaanza kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa ajili ya shughuli za maendeleo, baada ya Serikali kuagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu pamoja na wazee katika zoezi la kuunganishiwa umeme kwa kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA).
Umeme tayari ni kifaa ambacho akihitaji mtandao wa umeme katika nyumba isiyozidi vyumba viwili au kimoja ambapo humuwezesha mtumiaji kupata umeme kutoka kwenye nguzo na kumpunguzia gharama za kufunga mfumo wa umeme katika nyumba yake.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa maagizo hayo Februari 26, 2019 akiwa katika ziara ya kazi katika vijiji vya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambapo amesema kila wilaya nchini imepewa vifaa vya umeme tayari 250 ili kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini hasa watu wenye uhitaji maalum kama walemavu na wazee.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati inaeleza pia kuwa Mgalu ametaka taasisi za umma zipewe kipaumbele katika kuunganishiwa umeme kwa sababu zinahusika kutoa huduma muhimu za kijamii zenye manufaa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kifaa hicho kimegawanyika katika sehemu kuu tatu; kikata umeme (Sockect Braker), swichi kubwa (main switch), njia kuu tatu, taa moja kubwa na sehemu kuu sita za kupitisha umeme kwenda maeneo husika ya nyumba yako.
Kikata umeme (Sokect Braker) husaidia kupunguza madhara au itilafu yoyote isitokee katika nyumba, mathalani umeme ukija kwa wingi vifaa vya mteja haviwezi kupata athari.
“Swichi kubwa ni eneo liliopo kwenye umeme tayari ambalo linahusika na kuwasha, kuzima umeme na endapo shida yoyote itakapotokea inajizima yenyewe ili kuepusha uharibikaji wa vifaa au nyumba kuungua,” inaeleza Tanesco.
Soma zaidi: Maoni: Tunaweza kuwapatia furaha watanzania wengi zaidi kwa nishati jadidifu
Njia tatu za kifaa hicho zinaweza kutumika kwa matumizi tofauti tofauti kama ya kupikia na kupiga pasi. Ili mtumiaji apate kifaa hicho anatakiwa asiwe umbali wa mita 30 kutoka nguzo ya umeme ilipo na matumizi yake hayapishani na ya nyumba iliyofanyiwa mtandao wa umeme.
Agenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya 2030 inaeleza kuwa ulemavu hauwezi kuwa ni sababu au kigezo cha mtu kupata huduma muhimu za kijamii ikiwemo umeme kumuwezesha kufanya shughuli za maendeleo.
Wakati Serikali ikiendelea kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kwa kifaa cha umeme tayari, wadau wanaeleza kuwa kuna kila sababu ya kuangalia namna ya kutumia nishati jadidifu kuwawezesha walemavu na wazee kufanya shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kupata kipato kuendeleza maisha yao.