Mambo yatakayosaidia vijana kuchangamkia mikopo ya halmashauri
- Kukosekana kwa ari hiyo kunatokana na kukosa taarifa sahihi.
- Wengine wataja uoga wa kudaiwa kuwa sababu.
- Wadau washauri elimu itolewe kwa vijana.
Dar es Salaam. Kutokana na muitikio usioridhisha wa vijana kuchangamkia mikopo ya halmashauri za wilaya, Serikali na wadau wameshauriwa kuongeza elimu na kutoa taarifa sahihi ili kundi hilo liweze kufaidika na mikopo hiyo.
Mikopo hiyo inatolewa chini ya kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, sura 290 na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019.
Hiyo ni kwa mamlaka zote za serikali za mitaa Tanzania bara.
Kupata mikopo hiyo, inahitajika wanawake na vijana waunde kikundi cha watu wasiopungua watano huku watu wenye ulemavu wakitakiwa kuwa wanakikundi wasiopungua wawili.
Kikundi hicho kinatakiwa kiwe kimesajiliwa, kina akaunti ya benki yenye jina la kikundi na kijishughulishe na ujasiriamali au kiwe na kusudi la kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati.
Pia wanakikundi wawe Watanzania wenye akili timamu na watu wazima (18+), na kati ya wanakikundi, asiwepo mwenye ajira rasmi.
Licha ya uwepo wa fursa hiyo, bado mwitikio wa kuomba mikopo hiyo hasa kwa kundi la vijana ni mdogo tangu ianze kutolewa mwaka 2018/19.
Mikopo hiyo inatoka katika asilimia 10 ya mapato ya halmashauri.
Mikopo ya Halmashauri inanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Picha| Tanzania Web.
Ili kuondoa dhana zisizo sahihi kwa vijana, wadau wa masuala ya vijana wameshauri elimu itolewe ili vijana wajue kwa undani kuhusu mikopo hiyo.
Mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, Ben Bosco ameiambia Nukta Habari kuwa, ni mara ya kwanza anasikia juu ya mikopo inayotolewa na Halmashauri.
Kijana huyo amesema Serikali inatakiwa kuwekeza katika kampeni za kuelimisha juu ya mikopo hiyo na namna vijana wanaweza kuipata.
“Hamna elimu kuhusu hiyo mikopo kaka. Hatusikii hata tangazo wala post (bandiko) yoyote,” amesema Bosco.
Ili kuhakikisha wadau wa masuala ya fedha wanafanyia kazi suala hilo, wadau wengine wameshauri Serikali itoe takwimu za mikopo hiyo kwa mgawanyo wa makundi yanayonufaika badala ya kutoa takwimu za jumla.
Mratibu wa mradi wa Kijana Wajibika kutoka taasisi yamasuala ya vijana ya Restless Development, Badru Juma amesema ni vema Serikali ikatenganisha takwimu za utoaji mikopo hiyo ili kujua ni kundi gani linalobaki nyuma zaidi, nguvu iwekezwe kwenye kulielimisha.
“Zitolewe takwimu za mkopo umeenda kwa makundi mangapi ya vijana, mangapi yawanawake na mangapi ya watu wenye ulemavu,” ameshauri Badru.
Wanawake wamekuwa wakijiunga kwenye vikundi vywa wajasiriamali na kunufaika na mikopo. Picha| Gift Mijoe.
Vijana waelimishwe vigezo vya mikopo hiyo
Siyo kwamba vijana wote hawajui mikopo wala hawaiulizii. Wengine wanatamani kuipata lakini wanakuwa hawajakidhi vigezo vya kuipata.
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Karume anayesimamia soko la Ilala, Geraldina Bakalile amesema kwa eneo hilo, vijana wengi ni wafanyabiashara hasa mama ntilie na mafundi gereji lakini moja ya kigezo cha mikopo hiyo ni mtu kuwa mkazi wa eneo husika ili kurahisisha ukusanyaji wa marejesho.
Bakalile amesema kwa eneo la Karume, inakuwa ni ngumu kijana apewe mkopo wakati anaishi Kibaha au Bagamoyo.
“Ukimpa Sh15 milioni alafu akatokomea utaipataje, inabidi awe mkazi wa eneo husika. Hata kama akija na barua ya serikali za mitaa za eneo lake, siyo rahisi kuamini kwani baadhi ya watu hufoji,” amesema Bakalile.
Kiongozi huyo anashauri vijana kuchangamkia mikopo hiyo ambayo kwa sasa imenufaisha wanawake wengi.
Takwimu za Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zilizotolewa na Waziri Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha bajeti yake ya 2021/22 bungeni hivi karibuni alisema imetenga Sh64.5 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa vikundi 18,244 vya wanawake, vijana na Watu wenye ulemavu.
“Kati ya fedha hizo, Sh25.8 bilioni zilitengwa kwa ajili ya vikundi 8,223 vya wanawake, Sh25.8 bilioni kwa ajili ya vikundi 6,966 vya vijana na Sh12.9 bilioni kwa ajili ya vikundi 3,055 vya watu wenye ulemavu,” alisema Mwalimu Aprili, 2021.
Vijana watoa sababu za kutokuchangamkia mikopo
Baadhi ya vijana walioongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wamesema hawana elimu na taarifa za kutosha kuhusu mikopo hiyo.
“Sifahamu hata hiyo ni mikopo gani. Ila kwa jumla binafsi siko vizuri na mikopo. Siipendi,” amesema ni Mike Roosevelt, Mkazi wa Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Kijana huyo anaamini mikopo ni usumbufu hasa pale unapoanza kudaiwa marejesho.
Roosevelt amesema hata mikopo ya taasisi zingine za kifedha inahitaji mtu awe na dhamana na kwa kijana ambaye maisha yamempiga, hawezi kuwa na mali zisizohamishika ikiwemo nyumba, kiwanja na mengineyo kwa ajili ya kuchukulia mkopo.
Kwa vijana, mikopo ya halmashauri inaweza kuwafanya wafungue biashara zitakazoweza kuajiri na wengine. Picha| Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Vijana bado hawajatulia
Ili kupata mikopo hiyo, inatakiwa wanakikundi watokee katika kata na halmashauri moja na kwa mujibu wa vijana, ni changamoto kupata watu wenye ndoto sawa.
Mkazi wa mkoani Morogoro, Anna Kiando amesema vijana wapo kwenye umri wa kutafuta hivyo huwa wanajaribu mambo na “kuzikilizia kama yanatiki au laa”.
Amesema kuwapata watu watano na wakakubaliana kuwa na lengo moja ili kuchukua mkopo ni ngumu hasa kwa vijana ambao wanaogopa madeni tena ya Serikali.
“Ukimkuta mtu ukamwambia mkopo wa halmashauri anasema hataki kudaiwa na Serikali kwani jela ni nje nje akishindwa kurejesha. Wengi wanaona bora wakope kwa watu wanaowafahamu,” amesema Kiando.
Kwa mujibu wa Kiando, vijana wengi hukimbilia mijini kutafuta ajira na kila mtu anataka kuanzisha shughuli zake hivyo kufanya kazi kimakundi siyo hulka ya wengi.
Latest
