Serikali kujenga soko la kisasa Jangwani, wamachinga wakitoa kero zao
- Litasaidia wamachinga kupata eneo zuri la biashara.
- Ujenzi wa soko la Kariakoo unaendelea na baadaye Karume.
- Wamachinga walalamika kukosa wateja maeneo mapya.
Dar es Salaam. Serikali inakusudia kujenga soko kubwa katika eneo la Jangawani jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa mipango yake ya kuboresha mazingira ya biashara hasa kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga ambao walikuwa hawana maeneo rasmi ya kufanyia shughuli zao.
Mpango huo wa Serikali umekuja zaidi ya miezi mitatu baada ya Serikali kuwaondoa wamachinga katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo katika barabara kuu na kuwapanga upya katika masoko na maeneo mapya.
Hata hivyo, zoezi hilo liliibua changamoto kadhaa ikiwemo maeneo mapya waliyopangiwa kutokukidhi wingi wa wamachinga.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema anatambua changamoto hizo za wamachinga licha ya kuwashukuru kwa kukubali kupangwa upya na kuondoka barabarani, jambo liliboresha mandhari na muonekano wa maeneo mbalimbali nchini.
Amesema ili kutatua changamoto ya uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara, Serikali imeanza mchakato wa kuanza kujenga soko kubwa na la kisasa katika eneo la Jangwani jijini hapa.
Tayari amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kutafuta mkandarasi atakayejenga soko hilo kulingana na hali ya eneo hilo ambalo kila mwaka limekuwa likikumbwa na mafuriko hasa wakati wa mvua kubwa.
Sambamba na hilo ni ujenzi wa soko la Kariakoo lililoungua mwaka jana, ametoa fedha ili lijengwe upya ambapo wafanyabiashara waliokuwepo awali watarudishwa kuendelea na shughuli zao.
“Baada ya Soko la Jangwani ndipo tutaelekea Soko la Karume (lililoungua hivi karibuni) kwa sababu lazima katikati ya mji kuwe na masoko yenye miundombinu yote yatakayowezesha kufanya kazi masaa 24,” amesema Rais Samia leo Januari 25, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Ikulu jijini hapa.
Amesema pia Serikali ina mpango wa kujenga masoko makubwa pembezoni wa jiji hilo ili kukidhi mahitaji ya watu ambao hawawezi kuja katikati ya jiji.
Rais Samia amesema anaamii kuwa hiyo ni hatua kubwa ya kuwasaidia wamachinga kuwa kundi muhimu linalotambulika ambapo itakuwa rahisi kuwasaidia na kuwatambua katika shughuli zao na kuiwezesha Serikali kukusanya kodi.
Soma zaidi:
-
Soko la Soni: Kivutio kingine cha utalii wilayani Lushoto
-
Wafanyabiashara wasota na soko liloungua miaka saba Dar
- Wafanyabiashara wana la kujifunza kuungua soko la Kariakoo?
Wamachinga watoa kero zao
Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma) Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto amesema licha ya kutii agizo la Serikali kupangwa upya, zipo changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo ambazo zimeathiri shughuli za kundi hilo.
Amesema katika maeneo mapya waliopangiwa wanakabiliwa na changamoto ya miundombinu hafifu ikiwemo ubovu na barabara na ukosefu wa wateja.
“Baadhi ya maeneo mengi waliyopelekwa wamachinga hayana miundombinu rafiki kama barabara, vyoo na maji pamoja na sakafu, sambamba na ukosefu wa wateja kwa sababu ya kukosekana kwa route za daladala katika maeneo hayo,” amesema Namoto.
Katika baadhi ya maeneo hayo wamachinga wengine hawajapata kabisa maeneo ya kufanyia biashara, jambo liliwafanya waanze kushawishika kurudi tena barabarani.
Namoto ameiomba Serikali kuwaboreshea mazingira ya biashara zao, kuimarisha madawati ya machinga katika kila wilaya, kuwawezesha kupata uwakilishi katika vyombo vya maamuzi, na kutunga sera ya kuwatambua rasmi wamachinga.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inawatambua rasmi machinga kama kundi maalum, na litakuwa moja ya makundi maalum ambayo yatahudumiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum.