Suluhu ya kudumu majanga ya moto masoko ya Tanzania

January 18, 2022 1:39 pm · Maria
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalam washauri wafanyabiashara wafundishwe kukabiliana na moto.
  • Kuepuka makazi holela na kuhimiza miundombinu ya kisasa.
  • Bima na utekelezaji sheria upewe kipaumbele.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya soko la Karume lililopo Ilala Jijini Dar es salaam kuteketea kwa moto, wataalamu wa majanga wamependekeza kutolewa kwa na ujenzi wa masoko yenye miundombinu ya kisasa inayoweza kuepusha majanga mbalimbali ikiwemo moto.

Soko la Karume (soko la Mchikichini) liliteketea kwa moto usiku wa kuamkia Januari 16 mwaka huu huku chanzo cha moto huo kikiwa hakijulikani.

Moto huo uliteketeza sehemu kubwa ya soko hilo lenye wafanyabiashara zaidi ya 3,500 licha ya kazi iliyofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuudhibiti ili kunusuru mali za wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga.

Serikali imewataka wafanyabiashara wa soko hilo kuwa watulivu wakati ikiendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo iliyowaacha watu na machungu mbalimbali ikiwemo kupotelewa na mitaji.

Wakati Serikali ikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo ambalo limetokea mwanzoni mwa mwaka 2022, wadau na wataalam wa masuala ya mipango miji na udhitibiti wa majanga wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa elimu ya majanga inahitajika sana kwa wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa chama NSSR-Mageuzi, James Mbatia amesema kuwa moto ni miongoni mwa majanga ambayo yapo na yataendelea kutokea katika maisha ya kila siku, hivyo kunahitajika kutolewa elimu ya namna bora ya kujiandaa na kuwa tayari kupambana na majanga mbalimbali.

Elimu hiyo ielekezwe kwenye mfumo rasmi wa elimu na usio rasmi ili kuwapa urahisi wananchi wa kuweza kupambana na kujikinga na majanga ya aina hiyo.

Mbatia ambaye ana taaluma ya ukandarasi, amesema pia msisitizo unahitajika zaidi katika utekelezaji wa sheria zinazosimamia majanga ili kuwalinda wafanyabiashara na majanga ya moto.

“Kwakuwa sheria ya kuanzisha taasisi ya kupambana na kusimamia majanga ipo iliyotungwa 2015  (Disaster Management Act), Serikali inabidi iipe kipaumbele na utekelezaji sheria hiyo kwa kuanzisha  taasisi hiyo ya kupambana na majanga,” ameongeza Mbatia akizungumzia juu ya suluhu za majanga ya moto yanayotokea.

Ili kuhakikisha sheria inatekelezwa ipasavyo, ameshauri kuundwa kwa chombo maalum kitakachokuwa na kazi ya kuratibu shughuli za kujiandaa na kudhibiti majanga katika maeneo mbalimbali nchini.

Soko la Karume ni la pili jijini Dar es Salaam kutekeketea kwa moto ndani ya kipindi cha miezi mitano tangu soko la Kariakoo kuungua na kuwasababishia hasara wafanyabiashara.

Mtaalam wa utayari na udhibiti wa majanga, Masozi Nyirenda amesema kuwa kuna ulazima wa kuweka miundombinu rafiki kama vile njia na vifaa kwa ajili ya kukabiliana na majanga katika maeneo ya biashara ili kujiweka tayari na dharura yoyote inayoweza kutokeo ikiwemo moto.

Licha ya kuweka miundombinu hiyo, watumiaji wa masoko hawa wafanyabiashara waelimishwe kwa kina jinsi ya kukabiliana moto pale unapozuka ikiwemo kutumia vifaa vya kuzimia moto.

Nyirenda ambaye ni Meneja wa Miradi, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) amesisitiza kuwa utoaji wa elimu unatakiwa uwe endelevu na utolewe mara kwa mara katika sehemu za watu wengi huku akigusia suala la wafabiashara kuwa na bima ya biashara.

“Kuwepo na sheria kwa kila anayetaka kufanya biashara lazima akate bima ili janga linapotokea mfanyabiashara awe na pa kuanzia kuendelea na shughuli zake za maisha.Jeshi la zimamoto lipewe nguvu na kipaumbele katika bajeti zinazotolewa na serikali ili wawe na miundombinu na vifaa vya kutosha katika shughuli zao za udhibiti wa majanga mbalimbali,” amesema Nyirenda.

Kutokana na ukweli kuwa majanga ukiwemo moto yanaweza kutokea wakati wowote kuna umuhimu pia kuwa na sera nzuri zinazotekelezeka za upangaji miji kwa kuzingatia kanuni za kitaalam kupunguza athari za majanga zinapotokea. 


Soma zaidi:


Mtaalamu wa kujitegemea wa mipango miji, Rachel Emmanuel amesema kuwa Serikali  iweke juhudi katika suala la kupima na kupangilia vizuri masoko na makazi ili kuhakikisha hakutokei makazi holela hasa yanayohusisha shughuli za kibiashara.

“Uwepo wa miundombinu rafiki ni suala la kuzingatia sana katika sehemu za watu wengi kama masoko, miongoni mwa miundombinu inayohitajika sana ni masoko kupangiliwa kwa namna nzuri ambapo kutakuwepo na njia au barabara ambazo zitaruhusu magari ya Jeshi la Zimamoto kupita lakini pia uwepo wa matenki ya maji katika maeneo ya mikusanyiko,” amesema Emmanuael.

Amesema ikiwa matenki ya maji yatakuwepo sehemu za mikusanyiko kama vituo vya mabasi na masokoni itawapa urahisi Jeshi la Zimamoto katika shughuli za udhibiti wa moto iwapo utatokea.Amewashauri wafanyabiashara kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya majanga kwa kuzingatia taratibu za ujenzi na kuepuka kujiuganishia umeme kiholela huku wakiwekeza katika matumizi ya vifaa vya kisasa katika maeneo ya biashara. 

                        

Mipango ya Serikali

Baada ya moto huo wa soko la Karume, Meya Jiji la Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto amesema tayari wameanza mazungumzo na benki kuweka utaratibu mzuri wa kuhamasisha wafanyabiashara kwa wingi pamoja na kutoa elimu ya kukata bima.

Amesema ili kuhakikisha usalama wa wafanyabiashara wameanza kuwaamisha wafanyabiashara waliopo katika masoko yasiyo rasmi.

“Mfano mwishoni mwa mwezi huu tutawaondosha wafanyabiashara wa nyama katika machinjio ya Vingunguti, hadi sasa hivi tumewaacha pale kwa sababu tunamalizia soko la kisasa ambalo tumewajengea pale pale na tumelipa fidia Sh520 milioni,” amesema Kumbilamoto wakati akihojiwa na televisheni ya Clouds.

Mbali na hayo wafanyabiashara wa soko la Karume (Mchikichini) wameruhusiwa kuweka alama kwenye maeneo yao ili wajihakikishie usalama wakati wakisubiria ripoti ya kamati iliyoundwa kuchunguza chanzo cha moto uliosababisha kuteketea kwa soko hilo.

Uamuzi huo umefikiwa jana Januari 17, 2022 kwenye kikao kilichofanyika kati ya viongozi wanaowawakilisha wafanyabishara hao na Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DC), Ng’wilabuzu Ludigija baada ya maandamano yaliyofaywa kushikiza waruhusiwe kuingia kwenye eneo hilo kuendelea na shughuli zao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW