Rais Samia aungana na maelfu kumuaga Malkia Elizabeth II
- Anapumzishwa katika nyumba yake ya milele leo Septemba 19.
- Rais Samia aungana na viongozi wa dunia kutoa heshima za mwisho.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na watu mashuhuri kutoka kote ulimwenguni kutoa heshima ya mwisho kwa Malkia Elizabeth II jijini London kabla ya kupumzishwa katika nyumba yake ya milele.
Shughuli hiyo ya kumuaga Hayati Malkia Elizabeth II aliyetawala miaka 70 imefanyika huko Westminster Abbey.
Siku ya jumapili Rais Samia pamoja na viongozi wakuu wa kigeni takribani 500 walipata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa kusaini kitabu cha maombolezo kabla ya mazishi kufanyika kitaifa leo hii.
Tukio hili limekusanya maelfu ya watu waliomiminika katikati ya London usiku wa kuamkia leo huku baadhi wakishindwa kufika kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya usafiri wa treni.
Katika shughuli hiyo Mfalme Charles III amewaongoza wanafamilia ya kifalme nyuma ya jeneza la Malkia Elizabeth II huku ulimwengu ukiendelea kumkumbuka kwa mchango wake wa kuimarisha amani na utulivu duniani.
Mfalme mpya ameambatana na ndugu zake Prince Anne, Prince Andrew na Prince Edward, wakati Prince William na Prince Harry wakiweka kando tofauti zao na kushiriki mazishi ya bibi yao.
Soma pia
Wakati wa ibada ya mazishi, Askofu wa Canterbury amemsifu Malkia kwa “maisha tele na huduma ya upendo” na kuongeza “alikuwa na furaha, alipokuwa kwa wengi, akigusa maisha mengi.”
Malkia Elizabeth II anazikwa mahali pamoja na mpendwa wake Prince Philip, Duke wa Edinburgh, katika Kanisa la kumbukumbu la King George VI.
Inaaminika kuwa mazishi ya Malkia Elizabeth II yanakuwa “tukio kubwa zaidi la polisi kuwahi kufanywa” kwani mbali na maafisa 20,000 mjini London, wengine 2,300 wako kazini kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa Windsor mahali atakapozishwa.
Latest
