Halmashauri, wazazi wavutana shule kuwa ya “English Medium”

November 28, 2022 7:53 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Shule ya Msingi Nyanza B na C ambayo inakuwa ya binafsi inayotumia mtaala wa Kiengereza (English Medium). 
  • Wazazi wakataa watoto wao kuhamishiwa shule nyingine.
  • Halmashauri ya Jiji la Mwanza yasema itakaa na wazazi kupata muafaka. 

Mwanza. Mvutano umeibuka kati ya wazazi na Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya kutolewa kwa mapendekezo ya kuibadilisha Shule ya Msingi Nyanza B na C kuwa ya binafsi inayotumia mtaala wa Kiengereza (English Medium). 

Shule hiyo ambayo ilikuwa na shule tatu yaani A, B na C ambapo shule ya Nyanza A ilibadilishwa na kuwa Engilish Medium tangu mwaka 2020 kwa makubaliano ya kila mzazi atakayepeleka mtoto kuandikishwa kulipia ada ya Sh400,000.

Makubaliano mengine ni kuwa Shule ya Msingi Nyanza B na C haitaandikisha watoto wengine hadi waliopo watakapomaliza elimu yao ya msingi ndipo shule nzima itabadilishwa na kuwa ya English Medium.

Hata Hivyo, inadaiwa makubaliano hayo yamekiukwa baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na kamati ya shule kuja na mapendekezo mengine kuwa kuanzia Januari 2023 wanafunzi waliobaki kwenye shule hiyo watahamishiwa kwenye shule nyingine za Maendeleo, Nyakabungo na Makongoro.

Mapendekezo hayo ni baada ya wazazi kuandikisha watoto wengi katika shule ya English Medium ambapo hadi sasa shule hiyo ina jumla ya watoto 700.

Wakizungumza kwenye mkutano wa wazazi uliofanyika shuleni hapo hivi karibuni, baadhi ya wazazi wamektaa mapendekezo hayo na kuitaka kamati kuendelea na makubaliano ya awali ya kuacha wanafunzi wamalize kwanza shule kabla ya kufanya mabadiliko.

Ephrahim John ni mzazi wa watoto watano wanaosoma katika shule hiyo amesema wakati shule ya English Medium inaanzishwa makubaliano yalikuwa ni shule ya Nyanza A iboreshwe iwe ya English Medium wakati huo wanafunzi waliopo kwenye shule za Nyanza B na C hawataandikisha watoto wengine na waliopo hadi wamalize ndipo shule ibadilishwe yote.

“Wametugeuka, makubaliano hayakuwa hivyo tulipatana wanafunzi waliokuwa darasa la tatu katika shule hizo ndiyo wangekuwa wa mwisho kumaliza kwenye shule hiyo lakini sasa wametugeuka,” amesema John, mkazi wa Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza.


Soma zaidi:


Mkazi mwingine, Anjelika Sostenes amesema haungi mkono mapendekezo hayo kwa kuwa iwapo watoto watahamishwa na wengine wapo darasa la mtihani hawataweza kufanya vizuri.

Amesema tayari walimu wanaowafundisha wamewazoea hivyo kubadili mazingira itawasababisha washindwe kufanya vizuri.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Mtaa wa Uhuru, Bashe Shaban amehoji nini kimewasukuma kutaka kuibadilisha shule hiyo kwa haraka hivyo wakati makubaliano ilikuwa ni wanafunzi waliopo darasa la tatu hadi wamalize.

“Je, ni tamaa za hela kwa kuwa kumekuwa na ongezeko la wanafunzi? Au uhaba wa madarasa?,” amehoji Shaban. 

Shaban anasema kama shida ni upungufu wa vyumba vya madarasa ni vyema wakapandisha kiwango cha ada ili ipatikane fedha ya kujenga ghorofa kwa ajili ya watoto wanaotakiwa kuandikishwa.

Akizungumza kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Mirongo, Hamidu Suleiman amesema hayo yalikuwa maendekezo ya kamati ya shule na uongozi wa jiji la Mwanza lakini wakaona ni busara kuyashusha kwa wazazi ambao watoto wao wanasoma hapo ili nao waweze kutoa maoni yao.

“Tulipokea mapendekezo yao na tutayafikisha kwenye kamati lakini kabla ya kwenda kwa wazazi tayari mikutano mbalimbali imeshafanyika kuzungumzia suala hilo ikiwemo ya hadhara na vikao vingine vya ndani na majibu yameshatolewa yanasubiri utekelezaji,” amesema Suleiman huku akielekeza suala hilo aulize Mkurugenzi wa jiji ndiye mwenye majibu sahihi.

Hata Hivyo, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilipomtafuta Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Yahya Sekiete hakuweza kupatikana kwa wakati kutokana na kuwa kwenye vikao. 

Pamoja na kusubiri kwa muda mrefu pale alipotafutwa tena hakuweza kutoa ushirikiano wa kutosha.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW