Maumivu vifaa vya shule vyapanda bei Mwanza
- Bei imeongezeka kwa Sh500 hadi 5,000 kutokana na vifaa.
- Wazazi walalamikia kulazimishwa na baadhi ya shule kulipia gharama za vifaa kwao kwa bei ya juu.
- Walimu watakiwa kuwapokea wanafunzi hata kama hawajakamilisha mahitaji husika.
Mwanza. Muhula wa masomo kwa mwaka 2024 unatarajia kuanza kesho Januari 8, nchini Tanzania. Hali inayosababisha uwepo wa pilika pilika nyingi za wazazi kuhakikisha wanawanunulia watoto wao vifaa muhimu vitakavyowawezesha kuhudhuria masomo.
Kwa baadhi ya wazazi hususan waishio mkoani Mwanza wiki hii ni ya maumivu kwao kutokana na kupanda kwa vifaa vya shule sokoni, huku wengine wakitoboa mifuko yao zaidi wakilazimishwa kuvinunua katika shule wanapowapeleka watoto wao.
“Kwa kweli vifaa vipo juu, wapo waliopandisha sana na wengine wanauza bei ya wastani lakini kiujumla vifaa vya shule viko juu,” amesema Obadia Nyamabata aliyekuwa akinunua vifaa hivyo katika soko la Makoroboi jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Obadia, mwaka 2023 shati ya mtoto anayeingia darasa la kwanza liliuzwa Sh3500 ambapo sasa linauzwa kati ya Sh5,000 hadi 6,000 huku viatu vipanda kwa sh 5,000 kutoka Sh15000 ya mwaka 2023 hadi 20,000 mwaka 2024.
Vivyo hivyo kwa upande wa mabegi ya shule nayo yamepanda kutoka Sh20,000 na sasa yanauzwa sh25,000 hadi sh30,000.
Mahitaji mengine yaliyopanda bei ni pamoja na daftari za watoto zenye kurasa 200 zilizokuwa zinauzwa Sh1,000 na sasa zinauzwa Sh1,500.
Soma zaidi : Umemejua unavyowaokoa wafugaji na ukame Dodoma
Aidha, mbali na kupanda kwa gharama hizo wazazi na wafanyabiashara wamelalamikia baadhi ya shule hususani za binafsi kugeuka maduka ya vifaa vya elimu na sare za shule ambavyo huuza kwa gharama kubwa kuliko ilivyo sokoni.
Nyamabata amebainisha kuwa gharama ambazo wanazitoa kugharamia vifaa wangeweza kununua mahitaji mengine muhimu.
“Mfano unakuta sweta la shule linauzwa Sh30,000 shuleni wakati sokoni linauzwa kati ya Sh15,000 au Sh20,000 hiyobinayobaki si unaweza kununua kitu kingine,” amefafanua Nyamabata.
Kauli hiyo pia imeungwa mkono na Josephat Warioba, mfanyabiashara wa viatu katika soko hilo ambapo amebainisha kuwa jambo hilo linaathiri mwenendo wa biashara zao kwa kiasi fulani kwa kuwa wazazi hawanunui tena mahitaji kwao bali wanapeleka fedha shuleni.
“Unakuta biashara hamna kwakuwa vifaa vyote kuanzia viatu, soksi hadi sare za shule zipo shuleni mzazi anachotakiwa ni kupeleka hela hivyo kwetu sisi wafanyabiashara inakuwa vigumu,” amesema Warioba.
Serikali yatoa neno
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, amewataka walimu wilayani humo, kuwapokea wanafunzi hata kama watakuwa hawana mahitaji yaliyoainishwa ikiwemo sare na michango ili kuwapa nafasi wazazi wao kukamilisha mahitaji hayo.
Masala aliyekuwa akizungumza na wadau wa elimu wilaya humo alibainisha kuwa anataarifa za baadhi ya wakuu wa shule kuandika mambo yasiyo ya muhimu kwenye fomu za kujiunga na shule hali inayosababisha wanafunzi kushindwa kujiunga na masomo kwa wakati.
Soma zaidi : How pottery boost women incomes in Iringa region
“Tunaposema elimu bure sio kumrundukia mzazi mahitaji mengi ambayo yanasababisha ashindwe kumpeleka mtoto shule na kwa sababu hiyo watoto wengi wanachelewa kuripoti shule hivyo kuwe na utaratibu maalum wa kuwapokea watoto wanapoenda kuanza shule,”amesema Masala.
Aidha, amewataka maafisa elimu kuhakiki fomu za maelekezo ya kujiunga (joining instruction) zilizoenda kwa wazazi ili kujiridhisha kama mahitaji yaliyoandikwa humo ni muhimu kwa mustakabali wa mahitaji ya shule husika.