Watoto wa mikoa hii 5 ndiyo wanaoongoza kupata malaria Tanzania
- Ni Tabora, Kagera, Mtwara, Shinyanga na Mara.
- Maambukizi yanawahusu watoto walio chini miaka mitano.
Dar es Salaam. Tabora ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo watoto wake walio chini ya miaka mitano 5 wanaongoza kwa kupatwa na Malaria baada ya ripoti mpya kueleza kuwa karibu robo ya watoto wa mkoa huo walikutwa na maambukizi ya ugonjwa huo mwaka jana.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 (TDHS-MIS) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha kuwa Tabora inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha Malaria kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59 (kwa watoto wa chini ya miaka mitano) kwa asilimia 23 kwa kutumia kipimo cha papo kwa papo (RDT).
Kiwango hicho cha maambukizi cha mkoa huo mkubwa kuliko yote Tanzania kwa jiografia ni takriban mara tatu ya wastani wa kitaifa.
Utafiti huo ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano umeeleza kuwa wastani wa kitaifa wa maambukizi ya Malaria kwa watoto chini ya miaka mitano mwaka jana ulikuwa asilimia nane ukiongezeka kidogo kutoka asilimia saba ya mwaka 2017.
Tabora imefuatiwa kwa karibu na Mtwara ambao asilimia 20 ya watoto wake walipata maambukizi ya Malaria mwaka 2022, Kagera (asilimia 18), Shinyanga (asilimia 16) na Mara asilimia 15.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa unapotafsiri mwenendo wa Malaria, ni muhimu kuzingatia majira ya ukusanyaji wa taarifa za tafiti mbalimbali. Nchini Tanzania, kuna misimu mawili ya mvua, msimu wa vuli ambao huanza Novemba hadi Januari na msimu wa masika unaoanza Machi hadi Mei kila mwaka.
“Kwa kuzingatia utofauti wa majira ya mvua, mpangilio wa mvua, joto na hali ya unyevunyevu wa tabia nchi ya kitropikali nchini huchochea maambukizi ya Malaria kwa kipindi cha mwaka mzima,” imeeleza ripoti hiyo.
Wakati watoto wa mikoa hiyo wakiteswa zaidi na Malaria, Arusha, Dodoma, Singida, Kilimanjaro, Manyara, Songwe, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Mjini Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja ndiyo mikoa iliyokuwa na kiwango cha chini cha maambukizi ya Malaria kwa watoto.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo utafiti wake ulishirikisha wataalam kutoka Wizara ya Afya, maambukizi ya Malaria kwa watoto katika mikoa hiyo yalikuwa chini ya asilimia moja.
Uchambuzi wa ripoti hiyo unaonyesha zaidi kuwa Malaria inawatesa zaidi watoto walio chini ya miaka mitano waishio vijijini (asilimia 10.4) kuliko wale wa mjini (0.7).
Soma zaidi:
-
Vyandarua zaidi ya 700,000 kupambana na malaria Rukwa
- Watoto wa Kigoma waongoza kwa kuteswa zaidi na Malaria Tanzania – Ripoti
Licha ya wastani wa kitaifa wa maambukizi ya Malaria kwa watoto walio chini ya miaka mitano kuongezeka, kaya zenye chandarua angalau kimoja kilichowekwa dawa zimepungua hadi asilimia 74 mwaka 2022 kutoka asilimia 78 mwaka 2017.
Vyandarua vyenye dawa huzuia mbu kumuuma binadamu moja kwa moja na kumuua kwa kemikali.
“Matumizi ya vyandarua vyenye dawa vinaweza kupunguza idadi ya mbu waenezao Malaria na kusaidia kupunguza hatari ya Malaria katika ngazi ya jamii, na pia kwa mtu mmoja mmoja,” inaeleza sehemu ya ripoti.
Wakati utafiti huo unafanyika mwaka jana, asilimia 64 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano walilala kwenye chandarua kilichowekwa dawa usiku wa kuamkia siku ya utafiti.
Katika kaya zinazomiliki angalau chandarua kimoja kilichowekwa dawa, asilimia 81 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 walilala kwenye chandarua usiku wa kuamkia siku ya utafiti.
Latest
