Umemejua unavyowakwamua wanawake kiuchumi Tanzania

Esau Ng'umbi 0218Hrs   Disemba 30, 2023 Ripoti Maalum
  • Unasaidia upatikanaji wa nishati ya umeme unaotumika kwenye shughuli za uzalishaji zikiwemo saluni.
  • Wawezesha wanawake kujiajiri, kuchangia katika shughuli za maendeleo.

Dodoma. Kwa muda sasa, ulimwengu umeshuhudia kampeni za kuhamasisha usawa kijinsia katika matumizi ya fursa mbalimbali ikiwemo za kiuchumi na kijamii zikilenga kuongeza mchango wa wanawake ili kuchochea maendeleo endelevu nchini.

Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, inatafsiri dhana ya wanawake katika maendeleo kuwa ni hatua madhubuti za kujenga uwezo wa wanawake kujitegemea katika kufanya maamuzi na kuyatekeleza kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Sera hiyo inasisitiza kuwa maamuzi hayo hayapaswi kuingiliwa wala kubugudhiwa na mtu, chombo au taasisi yoyote kwa sababu tu wao ni wanawake.


Read more: From sunlight to harvest: Solar energy brings hopes to farmers in Iringa


Hata hivyo, baadhi ya ripoti zinabainisha kuwa, wanawake nchini Tanzania wamekuwa wakikumbana na changamoto katika safari yao ya kujikwamua kiuchumi, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nishati ya umeme katika maeneo mengi hususan ya vijijini, jambo linalokwamisha ushiriki wao kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Ripoti ya Pengo la Jinsia inayoandaliwa na Jukwaa la Kimataifa la Uchumi (WEF) ya mwaka 2023, inabainisha kuwa Tanzania ipo nafasi ya 48 kati ya 146 kwa ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, ambapo bado usawa katika matumizi ya rasilimali za nishati uko chini huku wanaume wakionekana kunufaika zaidi kuliko wanawake.

Aidha, Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati ya mwaka 2020 inaonesha kuwa ni asilimia 8.1 pekee ya kaya nchini Tanzania zinatumia vyanzo vya nishati safi kupikia. 

Katika asilimia 92 ya kaya zinazotumia nishati nyingine hususan kuni na mkaa, wanawake huwajibika zaidi kutafuta nishati ya kupikia ambapo wanabeba mzigo wa kukusanya kuni na kutumia teknolojia zisizo na ufanisi jambo linalo athiri afya zao, muda, na ufanisi.

Kituo cha kuzalisha umemejua uliosambazwa kwa wakazi wa Leganga wilayani Kongwa, kilichojengwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Elico Foundation. Picha l Esau Ng'umbi/Nukta Africa

Hata hivyo, angalau kwa sasa wadau wa nishati nchini Tanzania wamekuwa wakibuni miradi na programu mbalimbali zinazosaidia upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo ya vijijini, na kuwawezesha wanawake kujikita katika shughuli za uzalishaji.

Miongoni mwa wadau hao ni Shirika lisilo la Serikali la Elico Foundation, linalojihusisha na uendelezaji na usambazaji wa nishati jadidifu nchini Tanzania  hususani katika maeneo ya vijijini ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa.

Kupitia miradi yake ya gridi za umeme jua, ufungaji wa taa, ugawaji wa vifaa vya uzalishaji vinavyotumia umemejua kama mashine za kuunga vyuma, na majokofu, wamefanikiwa kuwawezesha wanawake kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Iringa.

Salome Nsomela, Mkazi wa Kijiji cha Leganga, wilayani Kongwa mkoani Dodoma ameiambia Nukta Habari kuwa kutokana na umemejua uliopo kijijini hapo anaweza kuingiza hadi Sh10,000 kwa siku kutokana na biashara mbalimbali anazozifanya.

“Naweza nikaoka mikate yangu kwenye jiko linalotumia umemejua, nikawauzia wananchi, kwa siku naweza kutengeneza mikate 50, ambayo ninauza mmoja Sh200,” amesema Salome ambaye awali alikuwa ni mama wa nyumbani asiye na shughuli ya kumuingizia kipato.

Pamoja na kuuza mikate, Salome ambaye ni mama wa watoto wawili, anatoa huduma ya kuandika na kuchapa taarifa mbalimbali, kazi inayomuingizia kipato cha ziada.

Wanawake wengine kijijini hapo kama Neema Mbagale (34) wametafuta fursa nyingine zitokanazo na umeme wa uhakika ikiwemo kufungua saluni za kike zilizowapatia ajira na kipato. 

Neema, ambaye saluni kwake ilikuwa ni ndoto ya siku nyingi, anasema anatumia mashine ya kuosha na kukausha nywele ya umeme jua, ambapo kwa siku anaweza kuhudumia wastani wa watu watano hadi sita anaowachaji kuanzia Sh2,000 hadi 5,000.

“Mwanzoni nilikuwa nasuka kawaida, sikuwa na ofisi maalumu, nilivyosikia kuna programu ya kuwezesha watu kiuchumi nikajiunga, na kwa sababu hapa kijijini hakukuwa na saluni mimi nikafungua hii,” anasema Neema ambaye ofisi yake iko umbali wa kilomita moja tu kutoka nyumbani kwa Salome.


Soma zaidi : Tanzania na mtihani wa kuongeza matumizi ya nishati jadidifu ifikapo 2025


Kupitia kipato kinachopatikana kwa kazi yake ya ususi, Neema amefanikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu kwake na kwa familia huku akijivunia zaidi kufanikiwa kukodi shamba kwa mara ya kwanza kwa kutumia faida anayopata.

Baadhi ya wanawake wao wameamua kutumia umemejua kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo.

Delina Uvambe, Mkazi wa Kijiji cha Lupembe Lwa Senga, mkoani Iringa anatumia mashine ya kumwagilia mazao inayotumia umeme jua, hatua iliyomuwezesha kupanua eneo la kulima, kuongeza mavuno pamoja na kuwa na afya njema.

“Awali nilikuwa namwagilia kwa mikono au nakodi mashine ya mafuta ambapo ilikuwa lazima ninunue mafuta ya lita tano, lakini mashine hizi zinatusaidia sana, tumepunguza gharama kubwa, tunapata mazao mengi kupita kipindi cha nyuma,” anasema Uvambe huku akitabasamu.

Kwa mujibu wa Delina, awali walikuwa wanatumia zaidi ya Sh25,000 kwa siku kwa ajili ya kukodi mashine pamoja na mafuta jambo lililoongeza gharama na kukwamisha shughuli za umwagiliaji kufanyika kwa wakati na hivyo kuathiri ukuaji wa mazao na hata mavuno.

Hivi sasa hali ni tofauti. Delina amefanikiwa kupanua shamba lake kutoka robo tatu ya ekari moja mpaka ekari mbili, huku akifanikiwa kujenga nyumba kwa kushirikiana na mumewe pamoja na kuchangia kwenye upatikanaji wa fedha za mahitaji mbalimbali ikiwemo ada za watoto wao katika kipindi cha miaka mitatu tangu alipoanza kutumia mtambo huo.

Mpaka sasa mtambo huo ambao walipewa bure na Shirika la Elico Foundation,  ni mali ya kikundi cha chapakazi kinachojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji, ambapo walikubaliana kuutumia kwa zamu katika mashamba yao na kila mwanachama hutoa Sh5,000 kila mwezi kwa ajili ya matengenezo.


Soma zaidi : Jinsi taasisi, mashirika yanavyoweza kukwepa mgao wa umeme Tanzania


Hata hivyo, pampu moja haitoshi kwa kuwa kikundi chao kina wanachama zaidi ya 20, jambo linalosababisha kuchukua muda mrefu kwa mwanakikundi mwingine kuipata kwa haraka kwa ajili ya kumwagilia mazao yake.

“Tuliwaomba Elico watuongezee mashine nyingine ili kupunguza msongamano, waliahidi kutupa mashine mwakani 2024, ingawa tumepanga pia kuwa na shamba la pamoja,” amesema Uvambe kwa bashasha.

Licha ya Ripoti ya Idadi ya Watu, Afya na Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS) ya mwaka 2022 kubainisha idadi ya wanawake wanaojishughulisha na kilimo imepungua kutoka asilimia 74.5 mwaka 2004/5 hadi 31 mwaka 2022, bado kundi hilo linatoa mchango mkubwa kwenye sekta ya kilimo hivyo wanapaswa kuendelea kuwezeshwa.

Mashine ya kumwagilia ya umemejua, inayotumika na kikundi cha chapakazi kilichopo Kijiji cha Lupembe Lwa Senga ambayo waliipata kutoka Shirika la Elico Foundation. Picha l Esau Ng'umbi/Nukta

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu (UNFPA) katika Mpango wake wa kuwawezesha wanawake kiuchumi katika kilimo limebainisha kuwa wanawake wanaojishughulisha na kilimo nchini Tanzania ni asilimia 67 dhidi 64 za wanaume.

Baadhi ya wadau wa nishati, wameishauri Serikali, jamiii pamoja na wadau wa nishati kuzingatia usawa wa kijinsia wakati wa usambazaji wa nishati ili kuhakikisha jinsia zote zinanufaika jambo litakalochochea kasi ya maendeleo.

Thabit Mikidadi, Afisa Miradi wa Mtandao wa Kijinsia na Nishati Endelevu wa Tanzania (TANGSEN) ameiambia Nukta Habari kuwa umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia unatokana na ukweli kuwa mahitaji ya nishati yanatofautiana kutokana na maumbile na mifumo ya kijamii.

“Unakuta mama anahitaji zaidi nishati kwenye kupika au kuchota maji, baba yeye anahitaji zaidi kwenye shughuli za uzalishaji kama kuendesha mitambo, lakini baadae wote watahitaji nishati kwa ajili ya mwanga, au kupata habari,” anaeleza Mikidadi.

Katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, Mikidadi amesema wameanzisha mpango wa miaka minne uitwao “Mpango wa Usawa wa Kijinsia Katika Upatikanaji wa Nishati Safi na Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania” unaolenga kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kuongoza na kunufaika na upatikanaji wa nishati.


Soma zaidi : Faida za kuzingatia usawa wa jinsia katika upatikanaji wa nishati Tanzania


Related Post