Zingatia haya unapompeleka mtoto shuleni kwa mara ya kwanza
- Inashauriwa kumuandaa mtoto wako kisaikolojia.
- Kama mzazi, unashauriwa kutembelea na kuifahamu vizuri shule.
- Kama mtoto wako anahitaji uangalizi wa kiafya, sema mapema.
Dar es Salaam. Ni msimu wa mwanzo wa mwaka ambao watoto wa rika tofauti wameanza kwenda shule wakiwemo wa madarasa ya awali.
Baadhi ya wanafunzi wa madarasa ya awali huanza shule mapema hata kuanzia miaka miwili na kupelekwa katika vituo maalum (Day Care Centres).
Licha ya kutaka mtoto aanze masomo, kama mzazi kuna mambo ambayo unatakiwa kuzingatia ili mtoto wako awe salama na kusudi la kumpeleka shule litimie.
Kwa mujibu wa Shirika la masuala ya elimu ya watoto, Start Early, kabla ya kumpeleka mtoto kuanza shule, mzazi anatakiwa kuwa amemwandaa mtoto kisaikolojia ikiwa kuwa mbali naye na hata mtoto kuwa amezowea watu wengine tofauti na mzazi.
Start Early inashauri, ikiwezekana mzazi aanzishe uhusiano na mwalimu wa mtoto mapema ili isiwe mshangao na majonzi kwa mtoto kukutana na mtu asiyemjua tangu awali.
Mzazi anaweza kwenda kukaa na mwalimu akiwa na mtoto kwa muda ili mtoto amzoee mwalimu au mlezi wake.
Ukifanya hivyo kwa siku kadhaa, unaweza kuwa na amani ya kuwa mtoto wako halii shuleni kwa kukukosa.
Inashauriwa uhakikishe mtoto wako amezoweana na mwalimu/ mlezi wake. Picha| She Leads Africa.
Uzingatie nini kingine?
Kutembelea eneo la shule kabla ya kumwandikisha mtoto
Mkazi wa Kinyerezi, Esther Koloboi ameiambia Nukta kuwa, kitu cha muhimu ni kufahamu mazingira ambayo mtoto wako ataenda kujifunzia.
Kwa Koloboi kitu cha muhimu ni sehemu salama ya mtoto kuchezea na uwepo wa huduma muhimu kama vyoo safi na miundombinu rafiki.
“Nimehakikisha nimeenda shuleni wakati wanafunzi wapo wanasoma. Nimeangalia wingi wa watoto na kulinganisha na walimu waliopo ili nisje kuambiwa siku mtoto wangu haonekani,” amesema Koloboi.
Kwa mama huyo mwenye mtoto mmoja, jambo lingine la muhimu ni uwepo wa maji shuleni kuhakikisha usalama wa afya ya mtoto wake.
Umbali wa shule na nyumbani
Kwa siku za kwanza kabla ya mtoto kuzoea mazingira ya shule, huenda ukahitajika kuwa karibu na shule na kama siyo wewe, basi msaidizi wako wa nyumbani.
Inashauriwa kutafuta shule ambayo unaweza kumfuata mtoto pale mambo yanapokuwa ndivyo sivyo.
Mkazi wa Dodoma, Simon Mmbaga amesema alichozingatia yeye ni kuhakikisha shule anayompeleka mwanaye ni ya mwendo wa kutembea kutoka nyumbani.
“Ndiyo kwanza anaanza shule, hivyo natakiwa kumpeleka shule ya karibu na nyumbani ili hata akisumbua huko shule iwe rahisi kutembea kwenda kumchukua au kukaa naye kwa muda,” amesema Mmbaga.
Soma zaidi:
- Ni sahihi watoto kupelekwa ‘twisheni’ wakati wa likizo?
- Sababu za wazazi kuwaongoza watoto kusoma vitabu
- Wazazi wafanye nini kudumisha mahusiano na watoto wawapo mbali?
Toa taarifa za mtoto wako kwa usahihi
Huenda ukawa na mtoto mwenye changaoto fulani ya kiafya ambayo inahitaji usimamizi wa matumizi ya dawa.
Inashauriwa kumpatia mwalimu au mlezi wa mtoto wako maelekezo ili mtoto wako aendelee kupata dawa zake hata bila ya usimamizi wako.
Mkazi wa Morogoro, Joyce Makonda ameiambia Nukta kuwa, kwa mtoto mwenye changamoto za kiafya ni muhimu kumwelewesha mwalimu au mtu yeyote atakayekuwa karibu na mtoto.
“Kwa mtoto wangu nimemwandikia mwalimu wake ratiba ya dawa yake. Nimechukua na namba yake ili nimpigie kumkubusha kila siku,” amesema Makonda.
Pamoja na hayo, inashauriwa kumpatie mtoto wako vitu vitakavyomkumbusha mazingira ya nyumbani ikiwemo mdori anayempenda zaidi na hata chupa ya kunywea maji.
Start Early inashauri mzazi kujua mtoto alichofundishwa ili akiendeleze nyumbani kwa ajili ya kuimarisha uelewa wa mtoto.
Latest
