Mzazi fanya haya kumuandaa mtoto na muhula mpya wa masomo mwaka 2023

December 26, 2022 7:57 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Fanya manunuzi ya vifaa vya shule na mtoto wako.
  • Fanya  vipimo vya afya kwa mtoto wako.
  • Mueleze matarajio yako.

Dar es Salaam. Kipindi cha mwisho wa mwaka huwa na pilikapilika nyingi kwa wazazi au walezi wenye jukumu la kusimamia taaluma ya mwanafunzi kuhakikisha wanarudi shuleni kuendelea na masomo yao.

Pilikapilika hizi huambatana na maandalizi ya aina mbalimbali ikiwemo ulipaji wa ada, ununuzi wa sare za shule, madaftari na pesa za matumizi yatakayomuweka mtoto kwenye hali nzuri akiwa shuleni.

Maandalizi hayo ni muhimu kwani yatamsaidia mtoto kupata elimu itakayomkomboa kifikra na kumsaidia kumudu mazingira yanayomzunguka.

Ili kumuandaa vema mtoto wako kabla ya kurudi shule kwa ajili ya msimu mpya wa masomo kwa mwaka unaofuata wa 2023 fanya mambo haya: 


Fanya manunuzi ya vifaa vya shule na mtoto wako

Mzazi unatakiwa  kupanga siku ambayo mtaenda pamoja na mtoto wako kununua vifaa vya shule na mahitaji mengine yanayohitajika kwa ajili ya masomo ya 2023.

Hii inamjengea mtoto hali ya kuwa na hamu ya kwenda shule na hasa akipata vitu ambavyo alikuwa anatamani kuwa navyo.

Kisaikolojia, mtoto huwa na shauku kubwa ya kwenda shule kama mzazi atamnunulia vifaa vipya vya shule ikiwemo nguo, viatu, madaftari na begi jipya.

“Ni wazi saikolojia ya mtoto anayeenda shule na vifaa vipya hawezi kuwa sawa na yule anayekwenda na vifaa vya zamani. Matamanio ya kurejea shule yanakuwa makubwa kwa yule mwenye vifaa vipya zaidi,” anasema Keneth Baga, mtaalam wa saikolojia na malezi ya watoto.

Kwa kuzingatia kupanda kwa bei za bidhaa hivi sasa, wazazi wananshauriwa kununua vifaa muhimu vya wanafunzi mapema kabla bei haijapanda zaidi.

Kaa na mwanao msimu huu wa sikukuu msikilize kuhusu ndoto zake na angalia namna unavyoweza kumsaidia kuzitimiza mwaka 2023. Picha | iStock/Unasplash.

Mfanyie uchunguzi wa afya yake 

Hakikisha unachunguza afya ya mtoto kabla hajaanza shule ili kipindi akiwa shuleni aweze kukomaa na masomo vizuri.

Kama uchumi uko vizuri nenda hospitali kamfanyie mtoto vipimo (Body checkup) hasa kwa wanafunzi ambao wanaosoma shule za bweni. Hii itamuhakikishia afya ya akili na mwili na kumuwezesha kumudu masomo kipindi chote anapokuwa shuleni. 

Daktari Emmanuel Shayo kutoka zahanati ya Arafa iliyopo Bunju A  jijini Dar es Salaam anasema kumfanyia mtoto vipimo kabla ya kurudi shule kutafanya mzazi kuwa na uhakika wa afya ya mtoto wake wakati wote awapo shuleni.

“Kabla mtoto hajarudi shule lazima apimwe damu, apimwe mkojo, minyoo na magonjwa mengine yanayoambukiza ambayo anaweza kwenda kuwaambukiza wenzake walio shuleni, “ anasema Dk Shayo.


Soma zaidi



Mueleze matarajio yako 

Kila mzazi au mlezi huwa na matarajio juu ya viwango vya ufaulu, uchaguzi wa tahasusi (course) za kuchukua kwa wanafunzi wa sekondari.

Mueleze umuhimu wa matarajio ambayo unayo juu ya masomo yake na namna gani ambavyo yatachangia kwenye kutimiza ndoto zake na kufikia malengo ambayo anayatamani.

Kwa wazazi wenye uwezo, Baga anashauri kuwaahidi zawadi watoto endapo watafanya sawa na matarajio yako. Inaweza kuwa viwango vya ufaulu ulivyowawekea au nafasi nyingine za kitaaluma unazotamani wafikie.

“Jambo hili humjengea shauku ya kurudi shule akiwa na ari mpya ya kujituma zaidi na kufikisha malengo,” anasema Baga.

Jipe muda wa kupata taarifa za shule anayosoma mwanao

Kwa kuwa ni mwaka mpya mzazi una jukumu la kutathmini shule anayosoma mtoto wako na hususani akiwa anaanza shule au umemuhamishia shule mpya.

Hii inaweza kumsaidia mzazi au mlezi kubaini kama mazingira ni mazuri kufanikisha ndoto za mtoto wake. Kama shule haina vifaa fulani vya kujifunzia mnunulie mwanao.

Kwa wanaoendelea na masomo, ni vema kujiridhisha na ratiba ya darasa jipya analoingia kama atahitaji kuwepo shule muda tofauti na darasa la mwaka 2022. Lakini inatakiwa kufahamu ni michango au mahitaji gani mengine yanahitajika shuleni. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV