Maarifa wanayohitaji wafanyabiashara wadogo kustawisha biashara zao

March 11, 2021 5:43 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na elimu ya Tehama ili kuwasaidia katika kupata masoko ya mtandaoni. 
  • Kingine ni elimu ya huduma kwa wateja na uwezo wa kudhibiti hasira na hisia zao.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa wafanyabiashara walio na misingi mzuri wa biashara hupata muda wa kujifunza mambo mawili matatu juu ya kustawisha biashara zao. 

Wapo ambao huenda mbali  na kuajiri wataalamu wa biashara na masoko kuwasaidia ili kuhakikisha wanapata faida wanayokusudia.

Hata hivyo, kwa upande wa wajasiriamali wadogo, huenda hawapati muda au hawana fedha za kuwawezesha kupata maarifa ya kitaalamu ili kukuza mitaji na biashara zao.

Jambo hilo huenda ni kati ya sababu ya biashara nyingi kufa au kudumaa bila kupiga hatua yoyote. 

“Kuna mama namfahamu ambaye alikuwa anauza mgahawa tangu nasoma shule ya msingi, na nilikua mteja wake. Mama yule hadi amezeeka, bado alikuwa anafanya kazi ile ile na hakuwahi kubadilisha chochote katika biashara yake zaidi ya kununnua vyombo,” amesema Awadh Saidi, mkazi wa Kimanga mkoani Dar es Salaam. 

Haikuchukua muda mrefu ambapo mama huyo alipata washindani wakubwa ambao walijenga migahawa mizuri na hivyo kuchukua baadhi ya wateja wake akiwemo Saidi. 

Hata hivyo, mama huyo hakushtuka wala kuboresha biashara yake ili kuendana na ushindani.

Kukosa elimu ya biashara na kufanya biashara kwa mazoea ni kati ya sababu za kushindwa kufanya vitu vikubwa kwa wajasiriamali wadogo na hivyo kuwa sababu ya kushindwa kuendelea. 

Haijalishi ukubwa wa biashara yako, bado unahitaji kuwa mkarimu kwa wateja wako. Picha| K15 Photos.

Ni maarifa gani wanayohitaji wajasiriamali hao ili kuzikuza biashara zao?

Huduma kwa wateja

Siku za hivi karibuni mimi na dada yangu tulienda gengeni kununua parachichi kwa ajili ya chakula cha mchana. Tulihitaji parachichi kubwa kwa ajili ya watu wanne na tulimwambia muuzaji hitaji letu. 

Baada ya kupewa parachichi dogo, dada yangu alimuuliza muuzaji, “hili litatutosha watu wanne?” muuzaji akajibu kwa hasira, “hiyo siyo kazi yangu, umeniomba parachichi nimekupa,” 

Hivyo ni kusema, muuzaji huyo hana huduma nzuri kwa wateja wake na hivyo huenda ikawa inamfukuzia wateja wengi. Haijalishi biashara au kazi unayofanya, ukiwa na lugha mbaya kwa wateja wako, itakuwia vigumu kufanya biashara.

Usafi na mazingira mazuri ya kazi

Endapo hauwezi kuweka eneo lako la kazi safi ikiwa ni kutumia vyombo visafi, kufuta meza baada ya mteja kumaliza kula na kudhibiti nzi katika eneo lako la kazi, hiyo ni changamoto.

Ni muhimu mfanyabiashara anayejiweza, atengeneze miundombinu mizuri ya usafi katika eneo lake la kazi ikiwa ni pamoja na vifaa vya kutupa taka na maji machafu au yanayotuama kipindi cha mvua.

Kwa kufanya hivyo, itakuwa rahisi kupata wateja kwani eneo lako la kazi litakuwa safi na salama kwa chakula.


Soma zaidi:


Ubunifu na kujitofautisha kibiashara

Mjasiriamalia kutoka Sise Chips Kinyerezi, Sise Christopher amesema wajasiriamali wanahitaji elimu ya ubunifu na kujitofautisha kibiashara kwani biashara nyingi zinazofanywa kwenye jamii zinafanana.

Christopher amesema wafanyabiashara wadogo hawataki kujaribu vitu vipya na kuthubutu kufanya makubwa na hilo huenda ndilo likawa chanzo cha biashara za baadhi yao kufungwa.

Mjasiriamali huyo ameshauri kuwa, wafanyabiashara wadogo wanahitaji elimu ili kujitofautisha na kuwa na uthubutu.

Yapo mengi ambayo wajasiriamali wanahitaji kufundishwa ikiwa ni pamoja na elimu ya tehama kwa ajili ya biashara na kutumia tehama katika kutafuta masoko. 

Hata hivyo, ili kufanikisha hilo inahitaji utayari na nia ya kubadilika na hivyo swali linabaki kwa wajasiriamli kuwa je, wapo tayari?

Enable Notifications OK No thanks