Zifahamu bei mpya za mafuta zinazotumika Tanzania Mwezi Juni

June 7, 2023 6:19 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya dizeli na mafuta ya taa yapungua huku ya petroli ikiongezeka
  • Mikoa ya kusini kuendelea kutumia bei za mwezi Mei
  • Wakazi wa Bukoba  ndio watanunua mafuta kwa bei ya juu zaidi mwezi Juni

Dar es Salaam, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) imetoa bei mpya za bei ya mafuta zinazopaswa kutumika mwezi Juni ambapo bei ya reja reja kwa mafuta ya taa na dizeli yaliyopokelewa  kupitia bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh209 kwa lita ukilinganisha na bei za mwezi uliopita.

Taarifa ya Ewura kwa umma kuhusu bei kikomo za mafuta zinazopaswa kuanza kutumika leo Juni 7 saa sita na dakika moja usiku zinaonesha bei ya mafuta ya petroli yaliyopokelewa bandari ya Dar es salaam pia, imeongezeka kwa Sh2 kwa lita ikilinganishwa na bei ya toleo la tarehe 3 Mei 2023.

Kwa muktadha huo wakazi wa Dar es salaam watanunua petroli  kwa Sh2,873, dizeli kwa Sh2,662 na mafuta ya taa kwa Sh2,829 kwa lita moja.

Kwa Mikoa ya Kaskazini yaani Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, bei ya rejareja ya mafuta ya dizeli kwa Juni 2023 imeshuka kwa shilingi 198 kwa lita  wakati bei ya mafuta ya petroli imeongezeka kwa shilingi 156 kwa lita ikilinganishwa na bei za toleo la tarehe 3 Mei 2023. 

“Kwa mafuta ya taa, waendeshaji wa vituo katika mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo kutokea bandari ya Dar es Salaam. Hivyo, bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo zitazingatia gharama za kupokelea mafuta hayo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,” inabainisha taarifa hiyo.

 Mikoa ya kusini kusalia na bei ya mwezi Mei

Kutokana na kutopokelewa kwa shehena yoyote ya mafuta katika bandari ya Mtwara mikoa ya Kusini yaani Mtwara, Lindi, na Ruvuma inaendelea kutumia bei ya rejareja ya mafuta ya dizeli iliyokuwa inatumika mwezi Mei.

Kwa mujibu wa Ewura  Kutokana na upungufu wa bidhaa ya petroli katika maghala ya kuhifadhi mafuta yaliyopo Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta katika mikoa ya kusini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo kutoka katika bandari ya Dar es Salaam hivyo bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa hiyo zimezingatia gharama za petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji.

Wakazi wa Bukoba mkoani Kagera ndio watakao nunua mafuta kwa bei ya juu zaidi mwezi Juni yaani Sh3,089 kwa lita moja ya petroli na Sh 3,044 kwa lita ya mafuta ya taa huku Mkoa wa Ruvuma wakichoma shilingi katika mafuta ya Dizeli ambapo watanunua kwa Sh3,085.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW