Zaidi ya Sh600 milioni kutatua changamoto ya umeme kisiwa cha Ijinga Mwanza

December 23, 2024 6:00 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo zitajenga miundombinu ya umeme jua katika kisiwa cha Ijinga.
  • REA wahimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mwanza. Serikali ya Tanzania imetenga zaidi ya Sh600 milioni kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umeme jua katika kisiwa cha Ijinga kilichopo wilayani Magu jijini Mwanza hatua inayotajwa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme katika eneo hilo. 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri na Nishati Dotto Biteko, aliyekuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Magu leo Disemba 23, 2024 amesema fedha hizo zitatatua changamoto hiyo kwenye vijiji zaidi ya 4,000.

“Mnavijiji 82, vijiji 81 vyote vina umeme kimebaki kijiji kimoja kipo kwenye kisiwa na tuliona itachukua muda kuwapelekea umeme kwa kulaza nyaya kwenye maji tukaona watu wa Ijinga ni Watanzania wanastahili kupata umeme…

…Tumetenga  milioni 619 ili nao wapate umeme,” amesema Dk Biteko aliyekuwa akipokea taarifa  ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi kwa mwaka 2024.

Naye Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Magu amesema kitendo cha kupeleka umeme kwenye kisiwa hicho kutachochea maendeleo.

“Kazi kubwa imefanyika, umeme sasa ni asilimia  99 tumebakiza kijiji kimoja tu cha Ijinga kwani vijiji 81 tayari vyote vina umeme,” amesema Kiswaga.

Wakazi Wilayani Magu wakipata elimu ya matumizi ya majiko sanifu yanayosaidia katika utunzaji wa mazingira ambayo kwa hivi sasa yanasambazwa na Rea. Picha| Mariam John.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameipongeza Serikali  kwa kuja na ajenda ya nishati safi ya Kupikia ambayo itaokoa mazingira na afya za Watanzania.

“Nawapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuibeba ajenda hii ya  Rais kwa kuandaa programu mbalimbali ikiwemo ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50,”  ameongeza Kiswaga. 

Kwa upande wake Ramadhani Mganga, Mhandisi wa Miradi kutoka REA aliyekuwa akizungumzia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa mwaka 2024/34  wanaendelea kuhamasisha wananchi wa eneo hilo kutumia nishati safi ya kupikia.

“Tumuunge mkono Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034,” amesema Mhandisi Mganga.

Jumla ya majiko 19,530 yatasambazwa katika Mkoa wa Mwanza ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks