YouTube yaja na sera mpya ya ufundishaji, ujifunzaji mtandaoni

September 10, 2022 6:08 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Inaanzisha kichezeshaji kwa ajili ya elimu katika jukwaa hilo. 
  • Kuwawezesha walimu na wanafunzi kuwa karibu zaidi.
  • Kitakuwa mbali na matangazo, viunganishi na mapendekezo.

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao umekuwa ukijifunza vitu mbalimbali YouTube basi una kila sababu ya kutabasamu kwa sababu mtandao huo umekuja mpango kabambe kwa ajili yako.

YouTube inayomilikiwa na kampuni ya Google jana Septemba 9, 2022 imezindua kipengele kipya ndani ya mtandao huo kwa ajili ya maudhui ya elimu.

Kipengele hicho kitatoa uwanja mpana kwa walimu na wanafunzi kujumuika pamoja na kuchagua kwa urahisi masomo wanayopenda kusoma. 

Pia YouTube imesema watakaotumia jukwaa hilo watakua huru dhidi ya matangazo ya kibiashara, viunganishi vya nje na mapendekezo ya aina yoyote.

 “Ili kuboresha matumizi ya YouTube katika mazingira ya elimu, tunazindua kichezeshaji cha Youtube kwa ajili ya elimu, kichezaji kipya kilichopachikwa kwenye YouTube ambacho kinaonyesha maudhui kwenye programu za elimu zinazotumiwa na watu wengi bila vizuizi kama vile matangazo, viungo vya nje au mapendekezo,” amesema Jonathan Katzman, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Bidhaa wa YouTube Learning.

Katika hatua za mwanzo YouTube imesema, inashirikiana na kampuni za elimu (edtech) nchini Marekani, zikiwemo EDpuzzle, Chuo Kikuu cha Purdue na Purdue Global.

Kichezeshaji cha elimu cha YouTube pia kitaboresha kichezaji kilichopachikwa cha YouTube katika Google Classroom kwa matumizi bora zaidi ya YouTube.

“Tunafurahi kuwa mshirika wa mapema wa YouTube ili kutoa kichezeshaji cha Elimu na dhamira zaidi ya EDpuzzle ni kuwasaidia wanafunzi kujifunza kupitia video,” amesema Quim Sabrià , Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza, EDpuzzle.


Zinazohusiana:


YouTube imepanga kufanya ushirikiano wa kujifunza kati ya wakufunzi na watazamaji wao kuwa mwepesi zaidi kupitia kichezeshi hicho kwa watakaolipia huduma wanaweza kuona video zao bila ya mwingiliano wa matangazo ya mtandaoni. 

“Mwaka ujao, watayarishaji waliohitimu wanaweza kuanza kutoa kozi bila malipo au kulipia ili kutoa uzoefu wa kina na uliopangwa wa kujifunza kwa watazamaji,,” imeleza YouTube.

Pia inaleta kipengele cha maswali kama njia mpya kwa watayarishi kusaidia watazamaji kupima maarifa yao na kuwasaidia wanafunzi kutumia yale waliyojifunza.

“Kwa mfano, watayarishaji wa hesabu wanaochapisha mfululizo wa aljebra wanaweza kuunda maswali kwenye kichapo cha jumuiya ili kuwauliza watazamaji wao maswali yanayohusiana na dhana iliyofundishwa katika video yao,”  imeelezea tovuti rasmi ya YouTube.

Pamoja na hayo mtandao huo umetoa toleo maalumu kwa Ukraine ili kuhakikisha raia wa nchi hiyo wanapata maudhui muhimu ya elimu, hata wakati vita ikiwa  inaendelea.

“Lengo letu ni kuendelea kurahisisha ujifunzaji kwenye jukwaa kwa kila mtu katika jumuiya, iwe ni watayarishi, wanafunzi darasani au wanafunzi kote ulimwenguni.

“Chochote unachotaka kujifunza baadaye, tunataka YouTube iwe hapo kwa ajili yako,” imeeleza YouTube kueleza namna mtandao huo unavyopanga kujumuisha wadau wengi zaidi wa elimu ulimwenguni kote.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW