Youtube yaleta mbinu mpya ya kudhibiti maudhui ya watoto mtandaoni
- Maboresho hayo yanamuongezea mzazi nguvu ya kudhibiti maudhui anayopaswa kuangalia mtoto mtandaoni.
- Wadau wanaamini maadili na malezi bora ni njia nzuri zaidi ya kumlinda mtoto na maudhui yasiyofaa.
Dar es Salaam. Mtandao wa kijamii wa Youtube umefanya maboresho kuwawezesha wazazi kudhibiti maudhui ambayo watoto wao wanaweza kuangalia katika mtandao huo kupitia simu au kompyuta.
Maboresho hayo ambayo ni mkakati wa kuimarisha mahusiano na wateja wake, wazazi wataweza kwenda kwenye kipengele cha udhibiti wa watoto ‘Parental Control’ na kumchagulia mtoto maudhui anayopaswa kuangalia.
Pia mzazi anapata fursa ya kupanga na kuchagua vipindi vinavyoendana na umri wa mtoto hasa vile vyenye kumjenga na kustawisha maisha yake, kadri atakavyoona inafaa.
Kupitia ‘Parental Control’ mzazi anaweza kuongeza maudhui ambayo angependa mtoto ayaangalie kwa kubofya kitufye + ambacho kinampa machaguo ya vipindi mbalimbali.
Lakini swali linabaki kuwa maboresho hayo yana maana gani katika malezi ya watoto? Ikizingatiwa kuwa mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya watoto kujifunza mambo mengi lakini wakati huo huo imekuwa ikiwapotezea malengo ya maisha kwa kuiga vitu visivyofaa katika jamii.
Zinahusiana: ‘Apps’ za elimu zinavyoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule.
Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa kumuongoza mtoto katika maudhui anayopaswa kuangalia katika mitandao ya kijamii ni njia mojawapo ya kumsaidia kimaisha.
Mtaalam wa Saikolojia, Gerald Ekoba amesema maboresho yaliyofanywa na Youtube ni hatua nzuri ya kuwalinda watoto kwasababu watoto ni zao la mazingira yanayomzunguka, “Ni hatua ya msingi, itasaidia katika maendeleo ya nidhamu ya mtoto kwasababu hiyo ndiyo inayomjenga katika njia inayostahili.”
Ikiwa mtoto ataelekezwa nini cha kuangalia Youtube inamjengea uaminifu kwa mzazi wake na kumuwezesha kuwa na afya nzuri ya akili katika maisha yake yote kwasababu baadhi ya maudhui ya Youtube yanaweza kumsababishia magonjwa ya akili.
Watoto ni kile wanachokiona katika jamii.|Ovation Internet.
Hata hivyo, kudhibiti maudhui siyo njia pekee ya kumlinda mtoto na hatari inayoweza kumkuta katika maisha yake lakini wazazi na jamii wanahitaji muda zaidi wa kukaa na watoto wao ili kufahamu changamoto wanazokutana nazo katika maisha.
Daktari wa Watoto katika hospitali ya Alafa Jijini Dar es Salaam, Dk Stella Emmanuel anaeleza kuwa ili kujenga mtoto kiakili ni vizuri kwa wazazi, walimu na ndugu wakae karibu na watoto wao ili kuwaepusha kuangalia vitu visivyowajenga na kujikita katika kuwapa vitu au kazi za msingi kutokana na umri wao.
“Watoto wanakua kwa ukaribu wa walezi, wazazi na walimu hivyo ni jukumu letu kuwalea watoto hawa katika mazingira yaliyo rafiki,” anasema Dk Emmenuel.
Malezi bora na miongozo ya kimaadili kwa watoto ni muhimu katika karne ya 21 ambayo matumizi ya mitandao ya kijamii kupitia simu za mkononi yameongezeka kwa kasi jambo linalotishia mstakabali wa watoto ambao ni rahisi kupokea maudhui bila kupima athari zake.
Mkazi wa Masaki Jijini Dar es Salaam, Verediana Mushi ambaye ni mzazi wa watoto wawili anasema amefaidika na maboresho ya Youtube kwasababu watoto wake ni hodari wa kutumia mitandao ya kijamii.
Anaamini njia sahihi ya kuwalinda watoto ni kuwapa muda wa kucheza na marafiki za0 ili kuwapunguzia muda wa kutumia simu au kompyuta, “Kama mzazi inanibidi wakati mwingine kuwapeleka katika sehemu tofauti kuwafundisha watoto mambo mbalimbali na kuongea nao kwa lugha wanazoweza kuelewa na kufundishika.”
Pamoja na jitihada zote za teknolojia kuwadhibiti watoto, bado jukumu la kumlinda na kumlea mtoto linabaki mikononi mwa mzazi au mlezi mwenyewe.