Wizara ya Ulinzi Tanzania kutumia Sh3.6 trilioni 2025/26
- Zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo kwenda katika matumizi ya kawaida.
- Bajeti ya wizara hiyo nyeti imeongezeka kwa takriban Sh320 bilioni.
Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limepitisha bajeti ya Sh3.645 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili iweze kutekeleza vipaumbele vyake kikiwemo uimarishaji uwezo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa vifaa vya kisasa.
Bajeti hiyo itakayoanza kutumika Julai 1, 2025 imeongezeka kutoka Sh3.326 trilioni ya mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la Sh319.7 bilioni.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha, Sh3.327 trilioni sawa na asilimia 91.3 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
“Sh318.8 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo,” amesema Dk Tax amewaeleza wabunge jijini Dodoma leo, Mei 20 2025.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) maarufu kama Ngome kupitia fungu 38 limetengewa Sh2.73 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh48.87 bilioni kugharamia shughuli za maendeleo.

Dk Tax amesema JKT imetengewa fedha za matumizi ya kawaida ShSh567.02 bilioni na shughuli za maendeleo Sh9.93 bilioni.
Wizara yenyewe, amesema imetengewa Sh26.36 bilioni kugharamia matumizi ya kawaida na wakati shughuli za maendeleo zikitarajia kugharimu Sh260 bilioni.
Licha ya ongezeko hilo, lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2025/26 limeendelea kubaki kuwa Sh87.6 milioni, sawa kabisa na lengo la miaka miwili iliyopita.
Bajeti kuimarisha uwezo wa JWTZ
Dk Tax ameleeza kuwa bajeti hiyo imelenga utekelezaji wa maeneo 10 ya vipaumbele yakiwemo kuimarisha uwezo wa jeshi kwa vifaa vya kisasa, kuboresha mazingira ya kazi na makazi ya wanajeshi, huduma bora za afya, mafunzo na matengenezo ya vifaa.
Amesema JKT itaendelea kuboresha miundombinu ili kuongeza uwezo wa kupokea vijana kwa ajili ya mafunzo ya uzalendo, ukakamavu, stadi za kazi na umoja wa kitaifa.

Katika mwaka huo wa fedha, juhudi zitaelekezwa katika kuimarisha viwanda vya kijeshi, taasisi za utafiti, na ushirikiano wa kimataifa kupitia mashirika kama Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya za kikanda.
Waziri Tax amehitimisha kwa kusema kuwa bajeti hiyo inalenga kulinda maslahi ya Taifa kwa kulinda miradi ya kimkakati, kutoa mafunzo ya ulinzi na kuimarisha mifumo ya utawala bora na huduma kwa watumishi wa jeshi.
Latest



