Polisi yawasaka wadukuzi baada ya kuzua taharuki mtandaoni
- Ni baada ya kudukua na kuchapisha maudhui kwenye baadhi ya akaunti za mtandao wa X ya Jeshi la Polisi na chaneli ya Youtube ya TRA.
Dar es Salaam. Maharamia wa mtandao wasiojulikana wemedukua baadhi ya akaunti za mitandao ya kijamii za taasisi za umma na binafsi ikiwemo ya Jeshi la Polisi na kuchapisha maudhui ya uzushi na yasiyo na maadili jambo lililozusha taharuki mtandaoni nchini.
Miongoni mwa akaunti zilizoathirika na shambulio hilo ni akaunti ya mtandao wa X (zamani Twitter) ya Jeshi la Polisi la Tanzania pamoja na akaunti ya mtandao wa Youtube ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taarifa za ajabu zilianza kuchapishwa kwenye ukurasa wa Jeshi la Polisi la Tanzania (@tanpol) mapema leo asubuhi majira ya Saa 1 asubuhi na baadaye kushamiri kuanzia majira ya saa 3 asubuhi.
Baadhi ya ujumbe uliochapishwa katika akaunti hiyo kabla ya kufutwa ulikuwa na maneno ‘Hack3d by Retards Inc. #ANTILARP #WHITEPOWER…”. Baadaye akaunti ilichapishwa mbashara maudhui ya uzushi yaliyokuwa yakitangaza kifo cha Rais Samia Suluhu Hassan jambo ambalo si kweli.
Polisi wawasaka waliochapisha uzushi
Mara baada ya watumiaji wa mtandao huo kuona taarifa hiyo na baadhi ya watumiaji wa mitandao kuanza kuzisambaza, Jeshi la Polisi, majira ya saa tano asubuhi, kupitia akaunti zake rasmi limetoa taarifa inayokanusha na kutoa maelezo yanayoashiria kuwa akaunti hiyo ilivamiwa hivyo kutaka umma kuzipuuza.
“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote aliehusika na utengenezaji na utoaji wa taarifa hizo na yeyote yule ambaye ataendelea kuzisambaza,” limesisitiza Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, muda mchache baadae chaneli ya Youtube ya TRA ilionekana kurusha maudhui yenye ujumbe sawa na uliochapishwa kwenye ukurasa wa mtandao wa X wa Jeshi la Polisi.
Mathalani, muda mchache baadae TRA kwa kutumia ukurasa rasmi wa mtandao wake wa X, kwa kupitia chapisho ambalo kwa sasa limefutwa imebainisha kuwa akaunti hiyo ilikuwa imedukuliwa na kuwataka watu kupuuza taarifa hizo wakati wakishughulikia kurejesha udhibiti wake.
Wadukuzi walionekana kutuma ujumbe wa wenye maudhui yanayofanana katika baadhi ya mitandao waliokuwa wamefanikiwa kuiingilia.
Kutokana na sintofahamu hiyo kujitokeza, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ametoa tahadhari na kukemea uhalifu wa mitandao akitoa onyo na kubainisha kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakaye bainika na kuhusika na vitendo hivyo.
Hata hivyo, Msigwa hakubainisha bayana kuwa kilichotokea ni shambulio la udukuzi ama la licha ya maudhui hayo kuchapishwa kwenye baadhi ya akaunti zinazofahamika kuwa ni rasmi.
“Imebainika kuwa kuna wahalifu ambao wanafungua akaunti za mitandao ya kijamii yenye majina yanayofanana na taasisi zinazoaminika na kuchapisha maudhui ya upotoshaji na yenye kuzua taharuki,” ameeleza Msigwa kupitia taarifa yake.
Baadhi ya wataalamu wa teknolojia wamewataka wasimamizi wa mitandao ya kijamii ya taasisi kuwa macho kutokana na mwenendo wa huo wa wadukuzi kuingilia mitandao.
‘Kuwa makini’
“Kuna wimbi kubwa la udukuzi linaendelea sasa…linalenga akaunti kubwa Tanzania,” Given Edward, Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya teknolojia ya Kinara Technologies amechapisha katika akaunti yake ya mtandao wa X.
Haya yanajiri ikiwa ni miezi michache tu ambapo Serikali kupitia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni kutangaza kuunda kikosi kazi cha kushughulikia masuala ya uhalifu wa kimtandao, na kuweka mazingira salama kwa wananchi ambao wamekuwa wakikabiliwa na uhalifu huo, ambao unaathiri shughuli zao za kiuchumi mnamo Novemba 2024
Kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Uhalifu na Ajali za Barabarani kwa mwaka 2023 iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha kuwa matukio ya uhalifu wa kimtandao yaliongezeka kutoka 1,006 mwaka 2022 hadi 1,369 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 36.1.
Baadhi ya watu wametapeliwa na uhalifu huo. Ripoti hiyo inabainisha kuwa wananchi walitapeliwa kiasi cha Sh5 bilioni kupitia uhalifu wa mitandao ambapo idadi ya matukio ya aina hiyo yaliongezeka kutoka matukio 2,951 mwaka 2022 hadi 3,731 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 26.4 .
Latest



