Sekta ya utalii yazidi kukua, Tanzania ikiongoza Afrika
- Watalii waongezeka kwa Asilimia 132 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024.
- Wizara ya Maliasili na Utalii yavuka lengo la mwaka 2025.
Dar es Salaam. Tanzania imerekodi ukuaji mkubwa katika sekta ya utalii na kuifanya kuwa nchi ya kwanza Afrika katika kasi ya ongezeko la watalii baada ya athari za maradhi ya Uviko-19 yaliyoitikisa sekta hiyo ulimwenguni.
Sehemu kubwa ya ukuaji huo ulirekodiwa mwaka wa 2024 baada ya kushuhudia ongezeko la watalii kwa asilimia 132, kutoka watalii 922,000 kwa mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.1 kwa mwaka 2024 kwa watalii wanaotoka nje ya nchi.
Mwenendo kama huo uliishuhudiwa katika utalii wa ndani ambapo watalii wa ndani waliongezeka kwa zaidi ya mara nne au asilimia 307 kutoka watalii watalii 788,000 kwa mwaka 2021 hadi watalii milioni 3.2 mwaka 2024 na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo.

Ongezeko hilo la watalii limeifanya Tanzania kupokea jumla ya watalii milioni 5.3 na kuiwezesha Wizara ya Maliasili na Utalii kuvuka lengo la Serikali la kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 kabla ya wakati.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa ongezeko hilo limechangiwa na maono ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii nchini kwa kutangaza vivutio kupitia njia mbalimbali ikiwemo ushiriki wake katika filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania.
“Katika kipindi hiki mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka, kutoka dola za kimarekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 3.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa, hatua hii imeifanya Tanzania kwa mujibu wa UN Tourism kushika nafasi ya tisa duniani na ya tatu barani Afrika kwa ongezeko la mapato, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya Uviko-19”, amesema Chana leo Mei 19, 2025.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism) zimebainisha kuwa Tanzania iliongoza kwa ukuaji wa sekta ya utalii katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 baada ya kurekodi ongezeko la asilimia 53 , Morocco (asilimia 32) na Algeria asilimia 17.
UN Tourism imeeleza kwenye toleo la ripoti yake inayoitwa World Tourism Barometer la May 2024, kuwa Afrika ilikaribisha asilimia 5 ya watalii wote duniani katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na watalii walioingia barani humu miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka 2023.
Latest



