Bajeti Wizara ya Ulinzi yapaa kwa mara ya nne mfululizo
- Bajeti ya mwaka 2022/23 yavuka Sh2 trilioni.
- Zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo kwenda katika matumizi ya kawaida.
Dar es Salaam. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inakusudia kutumia bajeti ya Sh2.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23, ikiongezeka kwa mara ya nne mfululizo tangu mwaka 2019/20.
Bajeti hiyo itakayoanza kutumika Julai 1, 2022 ambayo tayari imepitishwa na Bunge jana Mei 19, 2022 jijini Dodoma imeongezeka kutoka Sh2.3 trilioni ya mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la Sh355 bilioni.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa mara ya tatu mfululizo tangu ilivyoanza kuongezeka mwaka 2019/20 ambapo ilikuwa Sh1.8 trilioni
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya mwaka ujao, Sh230.3 bilioni sawa na asilimia 8.5 ya bajeti yote zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Kiasi kilichobaki ambacho ni zaidi ya asilimia 90 ya bajeti yote ndiyo kitatumika kutekeleza shughuli za kawaida za wizara hiyo nyeti nchini Tanzania.
Wizara hiyo ni miongoni mwa wizara chache ambazo zimepata kiwango cha juu cha fedha kutoka katika bajeti kuu ya Serikali ambayo inaratajia kuwa Sh41.1 trilioni.
Bajeti hiyo ya mwaka ujao wa 2022/2023 ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kabisa kwa wizara hiyo ndani ya miaka mitano iliyopita.
Zinazohusiana:
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019/2020
- Dk Mpango-Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
Ni bajeti ya matumizi ya kawaida
Dk Tax akihitimisha hotuba ya wizara yake alisema bajeti ya mwaka ujao itajikita katika maeneo 11 ya vipaumbele ikiwemo kuendelea kuliimarisha Jeshi kwa zana na vifaa vya kisasa, mawasiliano pamoja na rasilimali watu.
Fedha hizo zitatumika pia kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi wa Jeshi ikiwemo mafunzo, matunzo ya zana na miundombinu, maslahi, huduma bora za afya, ofisi na makazi na utatuzi wa changamoto za mipaka ya nchi na nchi jirani.
“Tutaendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia na kuendelea kulipa malipo na posho kwa wanajeshi, mishahara na stahili kwa watumishi wa umma,” alisema Tax.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) litajengewa uwezo kwa kuboresha miundombinu ili liweze kuchukua vijana wengi zaidi na kutoa mafunzo ya uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa, na stadi za kazi kwa vijana na kuliwezesha kujitosheleza kwa chakula kwa vijana wanaojiunga na mafunzo.
Uimarisha na kuratibu mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa kuhamasisha na kuelimisha wananchi juu ya masuala ya ulinzi, uzalendo wa kitaifa, usalama, na umuhimu wa kushiriki katika ulinzi wa nchi a kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya za Kikanda, na nchi mbalimbali katika nyanja za kijeshi na kiulinzi ni kipaumbele kingine.
“Kuendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura itapohitajika na kutatua migogoro ya ardhi kwa kupima mipaka ya maeneo ya jeshi, kufanya uthamini, na kulipa fidia ya ardhi iliyotwaliwa kutoka kwa wananchi kwa matumizi ya jeshi,” alisema Dk Tax.