Wizara ya Nishati yaomba kuidhinishiwa Sh2.24 trilioni bajeti 2025/26

April 28, 2025 5:58 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Kiasi hiki kimeongezeka kutoka asilimia 95.28 ya bajeti ya mwaka 2024/25 ambayo ilikuwa Shilingi trilioni 1.794.
  • Wabunge waiomba Serikali kuweka usawa wa bei ya kuunganisha umeme kati ya wananchi wa mjini na vijijini

Dar es salaam. Wizara ya Nishati imeliomba Bunge liidhinishe Sh2.24 trilioni kwa ajili ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 huku ikipanga kutumia asilimia 96.5 ya bajeti yake kwa miradi ya maendeleo.

Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko aliyekuwa akiwasilisha maombi ya bajeti ya wizara yake bungeni jijini Dodoma leo Aprili 28, 2025 amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha inayoombwa Shilingi trilioni 2.16 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Kiasi hiko kimeongezeka kutoka asilimia 95.28 ya bajeti ya mwaka 2024/25 ambayo ilikuwa Shilingi trilioni 1.794.

Biteko ameeleza kuwa kati ya fedha za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka huu, Sh 1.46 trilioni  ni fedha za ndani, na kiasi kinachosalia ni fedha kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wa matumizi ya kawaida, Serikali imetenga Sh79.2  bilioni sawa na asilimia 3.5 ya bajeti yote  ambayo imepungua  kutoka asilimia 4.72 ya bajeti ya mwaka uliopita ambayo iliyokuwa Sh 88.9 bilioni.

Kati ya fedha inayoombwa Shilingi trilioni 2.16 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Picha | Bunge la Tanzania.

“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha miradi ya maendeleo katika sekta ya nishati inatekelezwa kwa kasi zaidi ili kuchochea uchumi wa viwanda na ustawi wa wananchi,” amesema Biteko wakati wa kuwasilisha bajeti hiyo.

Kwa ujumla, bajeti ya Wizara ya Nishati imeongezeka kwa Sh363 bilioni sawa na asilimia 19 kutoka Sh1.88 trilioni mwaka 2024/25.

Itakumbukwa kuwa kiwango  cha bajeti kilichoombwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko Aprili 24, 2024  kwa ajili ya mwaka wa fedha ulioanza Julai 1, 2025 kilipungua kwa asilimia 38.2 kutoka Sh3 trilioni iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2023/24.

Gharama uunganishaji umeme zitazamwe upya

Hata hivyo, licha ya wabunge waliochangia wameunga kuunga mkono bajeti hiyo wameiomba Serikali kuweka usawa wa bei ya kuunganisha umeme kati ya wakazi wa maeneo ya vijijini na mijini.

Kwa sasa Serikali inaunganisha umeme kwa gharama ya  Sh321,000 kwa wakazi wa mjini na Sh27,000 kwa wakazi wa vijijini jambo linalolalamikiwa na wabunge hususan vigezo vinavyotumika kuamua iwapo eneo lipo mjini au vijijini.

Akichangia hoja ya bajeti hiyo Mbunge wa Kigoma mjini, Kilumbe Ng’enda amesema ni vyema Serikali ikawatazama wananchi wa mijini  baada ya kuwa imeweka nguvu kusambaza nishati hiyo maeneo ya vijijini.

Nge’nda amesema kuwasahau wananchi wa mjini ambao hawawezi kulipa Sh321,000 kunajenga tabaka na kuwakosesha huduma hiyo muhimu hoja iliyoungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjibi Jesca Msambatavangu aliyesema hali ya sasa inawakandamiza wananchi wa mijini wenye vipato duni.

“Ni kuwaonea wananchi wa mijini wenye kipato kidogo hivyo kuwanyima kupata fursa kama hizi za umeme” amekazia Msambatavangu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks