Rais Samia azindua Benki ya Ushirika Tanzania akihimiza mabadiliko

April 28, 2025 6:34 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema ni fursa kwa wakulima kupata mitaji na soko ili kuwekeza katika sekta hiyo.

Dar es salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezindua Benki ya Ushirika Nchini (Coop) huku akiitaka benki hiyo kuwa chachu ya mageuzi ya ushirika na kuwawezesha wakulima nchini.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa benki hiyo leo April 28, 2025  amesema benki hiyo ni hatua muhimu kwa wakulima kwa kuwa itawapa fursa ya kupata mitaji kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo, pamoja na kuwasaidia kupata masoko ya mazao yao ili kujikwamua kiuchumi.

Rais Samia ametoa wito kwa vyama vya ushirika kushirikiana na benki hiyo ili kupanua mtandao wake na kufikisha huduma katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa urahisi.

“Kasi ya kuongezeka kwa mitaji katika kilimo imekuwa ndogo ukilinganisha na sekta nyingine, uwepo wa benki hii kutaongeza upelekaji wa mitaji kwa wakulima na sekta nzima ya kilimo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametoa wito kwa vyama vya ushirika kushirikiana na benki hiyo ili kupanua mtandao wake na kufikisha huduma katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa urahisi. Picha | Ikulu

Hata hivyo, Rais Samia amesema pamoja na benki hiyo kuanzishwa ili kuchochea maendeleo ya ushirika bado ni inapaswa kufuata miongozo na taratibu iliyowekwa kisheria kama benki nyingine inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Aidha, Rais Samia ameoa wito kwa benki nyingine kutoiona benki ya Coop kama mshindani kwa kuwa imekuja kiongeza nguvu ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi hususan katika maeneo ya vijijini.

“Tushirikiane nayo, tufanye kazi nayo, najua biashara ya benki ni ushindani tunaweza kushindana nayo lakini kubwa tusaidiane nayo ili Watanzania waweze kunufaika na tuliyoyakusudia,” amesisitiza Rais Samia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Coop, Godfrey Ng’urah amesema kuanzishwa kwake kunaakisi utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya  mwaka 2020/25 inayotaka kukuza sekta za uzalishaji na ushirika.

Amesema mchakato wa uanzishwaji wa benki hiyo unatokana na kuunganishwa kwa Benki ya Ushirika Kilimanjaro na Tandahimba ambazo mwaka 2014-2020 zilikumbwa na changamoto ya ukwasi.

Kupitia benki hiyo mkulima ataweza kupata fedha za mauzo ya mazao yake mapema. Picha | Ikulu.

Baadaye amesema Serikali iliona haja ya kuwa na benki ya ushirika na ndipo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wa wakati huo, hayati Anna Mghwira alipoanzisha benki itakayosimamia ushirika.

Kwa mujibu wa Ng’urah benki hiyo inaanza ikiwa na matawi manne yaliyopo katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Kilimanjaro na Mtwara, na inashirikiana na mawakala 58 ambao ni vyama vya ushirika na Saccos mbalimbali ambapo bodi ya wakurugenzi inatarajia kufungua matawi mengine manne mwishoni mwa mwaka huu.

Benki ya Ushirika imezinduliwa ikiwa na mtaji wa Shilingi bilioni 58. Umiliki wa benki hiyo umegawanyika kwa asilimia 51 kwa vyama vya ushirika, asilimia 20 kwa Benki ya CRDB, asilimia 10 kwa Serikali, na asilimia 9 kwa wawekezaji wengine.

Aidha, Ng’urah amesema wameshasaini makubaliano na Bodi ya Stakabadhi Ghalani na wameanzisha programu maalumu ya kuhakikisha mkulima anapata fedha za mauzo ya mazao yake mapema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Abdulmajid Nsekela amesema wamefanya kazi kuhakikisha ushirika unaunganishwa katika mfumo wa kidijitali ili taarifa zake zipatikane kwa urahisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks