Idara ya Uhamiaji yakamata raia 62 wa kigeni Kariakoo

April 25, 2025 4:07 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Jumla ya raia wa kigeni 7,069 wakamatwa, uchunguzi wengine 305 waendelea.
  • 1,008 wafikishwa mahakamani, 703 wahukumiwa kifungo, 257 wahalalisha ukazi wao, huku 4,796 wakiondoshwa nchini.

Dar es salaam. Idara ya Uhamiaji nchini imekamata raia wa kigeni 62 waliokuwa wakiishi na kufanya biashara katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam bila vibali halali na wengine kukiuka masharti ya vibali vyao, katika ukaguzi maalum uliofanyika kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, imeeleza kuwa raia hao walikamatwa na kuondoshwa nchini baada ya kubainika kuwa walikuwa wanafanya shughuli za kiuchumi kinyume na taratibu za uhamiaji. 

Tukio hili ni sehemu ya ukaguzi wa kitaifa uliodumu kwa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili 2025, ambapo jumla ya raia wa kigeni 7,069 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa kwa makosa ya kukiuka sheria za uhamiaji. 

Kati yao, 1,008 walifikishwa mahakamani, 703 kati yao wakihukumiwa kifungo, 257 waliweza kuhalalisha ukaazi wao, huku 4,796 wakiondoshwa nchini. Aidha, uchunguzi bado unaendelea kwa watuhumiwa wengine 305.

Hatua hizi za Idara ya Uhamiaji zimekuja wakati ambapo kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani kuhusu ushindani usio wa haki unaotokana na raia wa kigeni kuendesha biashara ndogondogo zisizo stahili kuachiwa wageni.

Katika jitihada za kudhibiti tatizo hilo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, aliunda Kamati ya watu 16 Februari 2, 2025 kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya ongezeko la wafanyabiashara wa kigeni katika Soko la Kimataifa Kariakoo. 

Jitihada hizo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kudhibiti biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa.

Kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa Dk Jafo, Kamati hiyo iliundwa pia kufuatilia utoaji wa leseni kwa raia wa kigeni na wazawa, pamoja na kuanzisha kanzidata ya wafanyabiashara wote nchini ili kuwe na udhibiti madhubuti.

Aidha, zoezi la ukaguzi linalofanywa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama nchini linaendelea nchi nzima, huku mamlaka zikisisitiza kuwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika kukiuka taratibu na sheria za uhamiaji.

Idara ya uhamiaji imetoa wito kwa raia wa kigeni kuzingatia sheria na taratibu kutoka kwa mamlaka husika ili kuepukana na mkono wa sheria hasa katika wakati amabao idara hiyo imejipanga kuendeleza oparesheni kudhibidi wahamiaji haramu. 

“Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa raia wa kigeni kuzingatia matakwa ya masharti ya vibali vyao ili kuepuka hatua za kisheria au usumbufu unaoweza kujitokeza wakati huu ambapo zoezi la ukaguzi linaendelea,” imeeleza taarifa iliyotewa na na Idara hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks